DC OLE SABAYA AAGIZA TANESCO KUKATA UMEME OFISI ZA HALMASHAURI YA WILAYA YA HAI


Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ameagiza kukatwa umeme  ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya  Hai, mahali ambapo ofisi yake pia ipo hapo, kwa kile alichokieleza Halmashauri hiyo haijalipa bili ya Soko Kuu la Hai kwa muda wa miezi 2, na kuitaka TANESCO wakawashe umeme kwenye soko hilo.

Alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea soko hilo akimtaka Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) kurejesha huduma ya umeme sokoni hapo iliyoondolewa na shirika hilo kutokana na halmashauri kutolipa bili.

"DED (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya) na watu wako mnakuja kukusanya fedha kwa miezi mitatu mfululizo, mnasahauje kulipa bili kupitia fedha hizo?

"Hili nalo Rais asimamishwe aambiwe? Mimi na wewe tuwaombe radhi hawa wananchi, ila wakati huo nakuagiza Meneja wa Tanesco ukate umeme Ofisi ya Mkurugenzi na uwashe hapa sokoni na alipe deni hilo, na alipe bili za miezi sita ijayo.

"Umeme uwake hapa leo (jana) na 'go ahead' (maelekezo) ya kuwasha umeme kwa DED nitakupa baada ya kuona risiti. Na kwa kuwa ofisi yangu iko kwenye jengo hilo (la DED) tukapambane wote na hilo joto la kuwapuuza hawa wananchi tunaoambiwa kila siku kuwasikiliza na kuwahudumia."

Hata hivyo, Ole Sabaya alimweleza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Yohane Sintoo, kuwa hayuko tayari kufanya kazi kwenye ofisi ambayo haina huduma ya umeme na hayuko tayari kuona wananchi wanatozwa kodi ambayo hairudi kulipa deni la umeme.

Kutokana na agizo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo (Sintoo) alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo na kuwaomba radhi wananchi kutokana na kukatwa kwa umeme kwenye soko hilo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527