BUNGE LA RIDHIA MKATABA WA MINAMATA KUHUSU ZEBAKI


Na Lulu Mussa Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amesema inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 33 ya wachimbaji wadogo wa dhahabu hapa nchini, wameathiriwa na Zebaki kwa kupata magonjwa yakiwemo yale ya mifumo ya neva za fahamu, uzazi, upumuaji, figo, moyo, na udhaifu wa mwili.

Akiwasilisha azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki Simbachawene amesema, baadhi ya athari kwa mazingira zilizobainika kutokana na matumizi ya zebaki ni pamoja na kudhoofika kwa ukuaji wa viumbe hai wanaoishi ndani ya maji; uchafuzi wa mfumo mfuatano wa mazao ya chakula, mifugo na samaki; na uchafuzi wa vyanzo vya maji, hewa na udongo. 

“Lengo kuu la Mkataba huu ni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya Zebaki katika hatua za uzalishaji, matumizi na utupaji wake” Simbachawene alisisitiza.

Simbachawene ameainisha sheria ambazo zinatoa mwongozo wa jumla kuhusu usimamizi wa Zebaki ikiwa ni pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004); Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani (2003); Sheria ya Madini (2010); Sheria ya Afya ya Jamii (2009); Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (2003); na Sheria ya Chakula na Dawa (2003) na kusisitiza kuwa zitaandaliwa kanuni za Usimamizi wa Zebaki chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004) ili kuwezesha utekelezaji wa Mkataba huu.

Tafiti zinaonyesha kuwa zebaki hudumu katika mazingira kwa muda mrefu (miaka 2 hadi 20) na husafiri masafa marefu kwa njia ya hewa, maji (mito, maziwa na bahari) na udongo umbali hadi kilomita 1,000 kutoka kwenye chanzo; na kuathiri afya ya binadamu, viumbe wengine na mazingira. Athari hizi zinajitokeza zaidi katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea kutokana na nchi hizo kupunguza matumizi ya Zebaki. 

Awali akiwasilisha hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Suleiman Ahmed Sadiq amesema Kamati ianona umuhimu wa nchi kuridhia Mkataba huu kwa lengo la kushirikiana na nchi nyingine kutafuta suluhisho la zebaki bila kuathiri shughuli za wachimbaji wadogo.

“Ushauri wa Kamati ni kuwa Serikali ijitahidi kuhakikisha inapatikana teknolojia rahisi na rafiki kwa wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu” alisisitiza Mhe. Sadiq.

Zebaki ni miongoni mwa kemikali zinazohatarisha zaidi afya ya jamii duniani kutokana na kudumu katika mazingira kwa muda mrefu, kusafiri masafa marefu kwa njia ya hewa, maji (mito, maziwa na bahari) na udongo na hivyo kuathiri afya ya binadamu na mazingira. Jumla ya nchi 113 zimeridhia Mkataba huu ambao ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 16 Agosti, 2017 mara baada ya Nchi 50 kuridhia kama inavyotakiwa na Ibara ya 30 ya Mkataba wa Minamata.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post