WANAWAKE WANAOENDESHA VYOMBO VYA MOTO WAPEWA MAFUNZO KUKABILIANA NA AJALI BUKOBA

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Kagera,Winston Kabantega akitoa mada wakati wa mafunzo ya sheria na kanuni za usalama barabarani kwa wanawake wanaoendesha vyombo vya moto katika Manispaa ya Bukoba.

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog

Zaidi ya Wanawake 60 wanaoendesha vyombo vya moto katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamepatiwa mafunzo kuhusu sheria na kanuni za usalama barabarani ili kukabiliana ajali za barabarani.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mkurugenzi wa Lake Zone Driving School ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Kagera,Winston Kabantega yamefanyika Septemba 9, 2019 katika ukumbi wa Linaz uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Akifungua mafunzo,Kabatenga alisema mafunzo hayo yaliyokutanisha pamoja wanawake 64 yatadumu kwa muda wa  siku tano yakijikita zaidi katika kuzijua sheria za usalama barabarani,alama za barabarani,huduma ya kwanza, uzimaji wa moto, polisi jamii uongozaji wa chombo cha kila siku na sheria za madereva.

"Lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuwakumbusha akina mama kuzijua, kuzitambua sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali za kila mara zinazotokana na uzembe wa madereva na kusababisha watu kupoteza maisha huku baadhi ya familia kubaki yatima",aliongeza.

"Haya ni mafunzo ya kwanza kuwahi kutokea mkoani hapa,leo tumekutana hapa kwa awamu ya kwanza kwa akina mama kutoka Manispaa ya Bukoba. Akina mama wamekuwa hawana mwitikio wa ushiriki katika mafunzo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa kwani wanaume ndiyo wamekuwa wakijitokeza",alisema Kabatenga.

"Mafunzo haya yatawalenga akina mama hata wajasiliamali na watumishi wa serikali na mimi nimekuwa mdau mkubwa sana katika hili lakini nimeshuhudia mara kwa mara mwitikio wa akina mama ni mdogo sana ikilinganiswa na wanaume lakini ili kujua kuwa tumejipanga kikamilifu tutakwenda wilaya za Kyerwa Karagwe,Bihalamuro,Muleba, na Geita na hii ni katika kuwalenga akina mama tu waendesha vyombo vya moto" alieleza Kabatenga 

Amesema kuna makosa yanafanyika barabarani ni mengi yakiwemo ya kizembe hivyo mafunzo hayo yatasaidia kupambana na ajali za barabarani zinazotokana na uzembe.

Aliwahimiza akina mama hao kuchukua tahadhari wawapo barabarani ,kujali maeneo muhimu ya kuvukia watoto,wazee na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo alisema Madereva wanaokiuka sheria za barabarani baadhi yao ni wale ambao wana uzoefu wa miaka mingi barabarani lakini wameamua kujisahau matokeo yake wengi wao wameambulia kuwa walemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Kagera,Winston Kabantega akizungumza wakati akifungua mafunzo ya sheria na kanuni za usalama barabarani kwa wanawake wanaoendesha vyombo vya moto katika Manispaa ya Bukoba. Picha na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Kagera,Winston Kabantega akitoa mada wakati wa mafunzo ya sheria na kanuni za usalama barabarani kwa wanawake wanaoendesha vyombo vya moto katika Manispaa ya Bukoba.
Sehemu ya wanawake wanaoendesha vyombo vya moto katika Manispaa ya Bukoba wakiwa ukumbini.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527