WAZIRI WA KILIMO JAPHET HASUNGA AZINDUA MINADA YA KAHAWA KANDA YA MBEYA /SONGWE


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Serikali imewataka wakulima wote nchini kwa kupitia vyama vya Ushirika kuweka mkakati wa kununua na kutumia mitambo ya kuchakata kahawa ili kuongeza na kuwa na mwendelezo (Consistency) wa ubora wa kahawa inayozalishwa ili kupata bei nzuri mnadani au kwenye soko la moja kwa moja.

Waziri wa Kilimo amesema hayo Leo tarehe 22 Agosti 2019 wakati wa uzinduzi wa minada ya kahawa kanda ya Mbeya-Songwe na kuzitaka Halmashauri kupitia vyanzo vyake vya mapato kuendelea kuwekeza katika uendelezaji wa zao la kahawa ikiwemo uzalishaji wa miche, ununuzi wa CPU na kuwawezesha wakulima na maafisa ugani kupata mafunzo ya kilimo bora cha kahawa ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi.

Alisema kuwa ili kulinda ubora wa kahawa, matumizi ya mitambo ya kisasa ya kuchakata kahawa (CPU) hayawezi kuepukika. Alisema nchini kuna takribani mitambo 481 kiasi ambacho bado kipo chini ukilinganisha na kiasi cha kahawa inayozalishwa. "Hivyo nawasihi wadau wote muone umuhimu wa uwepo wa mitambo hii kwa kuwa ili upate kahawa nyingi zenye sifa za ubora unaofanana ni lazima kuwepo na matumizi makubwa ya CPU tena kwa kuzingatia hatua zote za uchakataji wa kahawa" Alikaririwa Mhe Hasunga

Mhe Hasunga aliongeza kuwa Lengo la Serikali ni kuona kwamba kahawa zote zinaandaliwa katika mitambo ya kisasa (CPU) ili zipate bei nzuri katika masoko kwani dhamira ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ni kuimarisha tija katika uzalishaji kadhalika kutafuta masoko ya mazao nje na ndani ya nchi.

Alisema kuwa Ili kuhakikisha tasnia ya kahawa inaondokana na changamoto ya tija ndogo na uzalishaji, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kuongeza kasi ya upatikanaji wa miche bora ya kahawa kupitia TACRI; Ruzuku ya miche inayotolewa na Bodi ya Kahawa na kuanzisha utaratibu wa upatikanaji wa mikopo ya mbolea kwa wakati kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Sekta Binafsi.

Aliongeza kuwa hatua hizo zimewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa kutoka tani 43,625 za kahawa safi msimu wa mwaka 2017/2018 mpaka kufikia tani 68,147 msimu 2018/2019.

Waziri huyo wa kilimo Mhe Hasunga alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa tija katika uzalishaji wa kahawa kwa wakulima wadogo wa kahawa ni ndogo sana ukilinganisha na wakulima wa mashamba makubwa na wakulima wa kahawa wa nchi nyingine. Aliongeza kuwa Wastani wa tija kwa mti mmoja wa kahawa ya Arabika ni gramu 350 ikilinganishwa na kilo moja (gramu 1,000) kwa nzi za Brazil na Vietnam.

Aliziraja Sababu kubwa zinazosabisha tija ndogo kwenye kahawa kuwa ni pamoja na Matumizi madogo ya mbolea na virutubisho kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji; na Wakulima kutokuzingatia kanuni za kilimo bora cha kahawa ambapo wakulima wengine hawatunzi kabisa miti yao ya kahawa na huvuna tu kile kitakachopatikana.

Sababu nyingine ni Uwepo wa magonjwa na wadudu waharibifu wa kahawa Miti iliyozeeka sana na kupoteza uwezo wa kuzaa vizuri; Badala ya kutumia miti iliyoboreshwa yenye uwezo mkubwa wa kuvumilia magonjwa na kuzaa sana. Nimeambiwa mti wa mmoja ulioboreshwa unao uwezo wa kuzaa wastani wa kilo 3 – 5 za kahawa kavu (Parchment).

Aidha, Mhe Hasunga amsema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya kahawa na kuhakikisha inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kupunguza umaskini, kuongeza pato la taifa na kuongeza ajira kupitia viwanda mbalimbali vya kahawa.

Moja ya lengo kuu la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuijenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ili kufikia lengo hilo, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeendelea kuhamasisha matumizi ya miche bora ya kahawa ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima, kuimarisha mazingira ya biashara na kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya kahawa ili kuiwezesha kutoa mchango unaohitajika katika kujenga Tanzania ya viwanda.

Kuanza kwa minada ya kanda ya kahawa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuwa kuanzia msimu wa kahawa 2019/2020 Bodi ya Kahawa ianze kuendesha minada ya kahawa katika Kanda nne (4) za uzalishaji wa kahawa. Kanda hizo ambazo minada ya kanda itafanyika ni Kanda ya Mbeya/Songwe mnada unafanyika Mbozi, Kanda ya Ruvuma/ Njombe mnada unafanyika Mbinga Mkoani Ruvuma, Kanda ya ziwa mnada unafanyika Bukoba Mkoani Kagera na Kanda ya Kaskazini mnada unafanyika Moshi Mkoani Kilimanjaro.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527