SERIKALI YAITAKA NIC KUCHANGIA PATO LA TAIFA KWA ZAIDI YA ASILIMIA TANO


 Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Bima la Taifa- NIC, Dkt. Elirehema Doniye (kulia), akikabidhiwa rasmi ofisi hiyo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo, Bw. Sam Kamanga, jijini Dar es Salaam.

 Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa- NIC, Bw. Sam Kamanga (kushoto), akitoa maelezo wakati wa kukabidhi rasmi ofisi kwa Mkurugenzi mpya wa Shirika hilo, Dkt. Dkt. Elirehema Doniye (wa pili kushoto).
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa- NIC, Bw. Laston Msongole, wakishuhudia makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika  la NIC. Bw. Sam Kamanga na Mkurugenzi Mtendaji mpya waShirika hilo, Dkt. Elirehema Doniye.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Bima Tanzania- NIC, Dkt. Elirehema Doniye, baada ya kukabidhiwa ofisi rasmi, jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa- NIC, Bw. Laston Msongole (kulia) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika hilo, Dkt. Elirehema Doniye, kabla ya kukabidhiwa rasmi Ofisi, jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akipeana mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa- NIC, Bw. Laston Msongole (kulia), baada ya kushuhudia makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo, Bw. Sam Kamanga (hayupo pichani) na Mkurugenzi mpya , Dkt. Elirehema Doniye (katikati), jijini Dar es Salaam.
(Picha na Peter Haule, WFM, Dar es salaam)Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imelitaka Shirika la Bima la Taifa- NIC kuhakikisha mchango wake unafikia zaidi ya asilimia tano katika pato taifa badala ya chini ya asilimia moja ya sasa ili kuweza kuchochea kasi ya ukuaji wa Sekta ya Fedha nchini. 
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, wakati akishuhudia kukabidhiwa rasmi Ofisi Mkurugenzi mpya wa Shirika la Bima la Taifa- NIC, Dkt. Elirehema Doniye.
Dkt. Kazungu amesema kuwa Shirika la NIC, linatakiwa kujipanga kimkakati kuwa chanzo kizuri cha mapato na kuhakikisha linawafikia wananchi wengi zaidi hususani katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Aidha amelitaka Shirika la NIC kuhakikisha linajipanga kiushindani kutoa bima ya miradi yote mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NIC, Bw. Laston Msongole, amesema kuwa Shirika hilo linawagusa watanzania wote kwa kuwa linatoa huduma zake Tanzania Bara na  Zanzibar.
Alisema kuwa Shirika la NIC, limeanza kufanya vizuri katika soko hivyo ni jukumu la Mkurugenzi mpya kuendeleza juhudi hizo kwa kuwa hapo awali lilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa, kwa kuona umuhimu wake Shirika hilo limebaki kuwa la wananchi na sasa linatakiwa kujiendesha kibiashara.
Naye Mkurugenzi mpya wa Shirika hilo Dkt. Elirehema Doniye, amesema kuwa anafanya jitihada kuhakikisha  Shirika hilo linaongeza ufanisi zaidi ili liweze kuchangia katika pato la Taifa kikamilifu kama alivyoelekeza, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa Shirika hilo linajiendesha kibiashara hivyo ni lazima watendaji kufanya kazi kwa nidhamu ya juu, kuwafikia wateja wadogo na wakubwa  na kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
Aidha aliyekuwa Mkurugenzi wa NIC, Bw. Sam Kamanga, amesema kuwa amemkabidhi Mkurugenzi mpya Shirika ambalo limeanza kufanya vizuri, kwa kuwa tayari kuna bima ya Kilimo ambayo itawafikia wananchi wengi, lakini pia  NIC imepata tuzo mbalimbali hivyo ni jukumu la uongozi mpya kuendeleza mafanikio hayo.
Mwisho

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527