BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA YATOA MKOPO WA SH. BILIONI 414 KUJENGA BARABARA ZA MZUNGUKO DODOMA


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Jiji la Dodoma na vitongoji vyake, hivi karibuni litabadilika mwonekano wake na kuwa la viwango vya kimataifa baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu ya dola milioni 180 sawa na shilingi bilioni 414 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za pete (ring road) kwa kiwango cha lami na uboreshaji wa miundombinu katika Jiji hilo.


Makubaliano ya mikopo hiyo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, kwa upande wa Serikali, na Meneja Mkazi wa Benki hiyo hapa nchini, Bw. Alex Mubiru.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mikopo hiyo, Bw. Doto James, amefafanua kuwa mradi utahusisha Ujenzi wa barabara ya mzunguko wa njia nne zenye urefu wa km 110.2 kwa kiwango cha lami kutoka Nala – Veyula – Ihumwa – Matumbulu.

Alisema mikopo hiyo pia inahusisha uboreshaji wa upatikanaji wa miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo huduma za maji na vituo vya afya; Ukarabati wa barabara za mchepuko; na Utekelezaji wa mikakati ya usalama wa barabarani katika mji wa Dodoma itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili” alifafanua Bw. James

”Kupitia Mikataba hii, Benki ya Maendeleo ya Afrika itatoa kiasi cha dola za Marekani milioni 138 kupitia dirisha la Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB Window) na dola za Marekani milioni 42 zitatolewa kupitia mfuko wa Africa Growing Together Fund (Mfuko wa Serikali ya China unaosimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika)” alisisitiza Bw. James

Aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za uwekezaji katika miundombinu ya usafiri itakayoiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Uwekaji saini wa Mikataba hii miwili itaongeza kiasi cha fedha ambacho kimetengwa na Benki kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara nchini Tanzania, kutoka dola za Marekani milioni 858.16 hadi dola za Marekani bilioni 1.038, sawa na takribani sh. trilioni 2.39”, aliongeza Bw. James

Alisema Barabara hiyo inaungana na barabara ya Cape hadi Cairo inayojulikana kama the Great North Road Highway yenye urefu wa km 10,228 inayopita katika nchi nane ambazo ni Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Zambia, Tanzania, Kenya, Ethiopia, Sudan na Misri na ni barabara ya ukanda wa kati (central corridor) inayounganisha Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Uganda.

Alidokeza pia kuwa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeonesha  utayari wa kufadhili ukarabati wa barabara ya Bagamoyo–Pangani-Tanga kwa kiwango cha lami na Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa-Msalato, utakaojengwa mkoani Dodoma  ambapo tayari maandalizi yameanza.

Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB), Bw. Alex Mubiru, alisema kukamilika kwa mradi huo kutaiunganisha Dodoma na mikoa mingine ikiwemo Arusha, Iringa, Singida, na Dar es salaam na kwamba utasaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dodoma kwa sababu magari yanayokwenda kwenye maeneo hayo yatapita pembezoni mwa Jiji.

“Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na washirika wake tutatoa asilimia 84 ya gharama za mradi ambazo ni dola za Marekani Milioni 215 wakati Tanzania itatoa asilimia 16 na baadae mwaka huu tutatoa kiasi kingine cha msaada wa takriban dola milioni 7.2 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuimarisha mazingira kwa kupanda miti kwenye eneo la mradi” alisema Bw. Mubiru.

Aliongeza kuwa hivi sasa Benki yake inajiandaa kutoa mkopo kwa ajili ya miradi miwili muhimu ukiwemo mradi wa uboreshaji wa  barabara kutoka Bagamoyo-Pangani-Tanga-Horohoro/lunga, Lunga – Mombasa-Malindi pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa-Msalato, miradi ambayo Bodi ya Benki hiyo inatarajia kuipitisha mwishoni mwa mwaka 2019.

Meneja Mkazi huyo wa AfDB nchini alisema matukio haya yote yanatokea kwa sababu Benki yake ina imani na kupongeza mafanikio makubwa ya Serikali ya Tanzania katika kuimarisha maendeleo ya watu wake na kwamba Benki hiyo iko tayari kuhakikisha azma hiyo inafikiwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post