YALIYOJIRI WAKATI WA SAFARI YA RAIS MAGUFULI KUTOKA KARAGWE MKOANI KAGERA KWENDA CHATO MKOANI GEITA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imechukua hatua madhubuti za kuwalinda wakulima wa zao la kahawa kwa kutoa fedha ili kuviwezesha vyama vya ushirika kununua kwa bei nzuri na ameruhusu wanunuzi binafsi wa ndani na nje ya nchi kununua kahawa hiyo ilimradi wazingatie sheria na utaratibu uliowekwa na Serikali.



Mhe. Rais Magufuli amesema hayo  tarehe 11 Julai, 2019 alipozungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamishenye, Kemondo, Muleba na Kyamyorwa Mkoani Kagera wakati akiwa safarini kutoka Karagwe kwenda Chato Mkoani Geita.

Amefafanua kuwa hatua ya Serikali kutoa fedha kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambapo wakulima wanauza kahawa yao kupitia vyama vya ushirika kwa bei ya shilingi 1,100/- kwa kilo imelenga kukabiliana na unyonyaji dhidi ya wakulima uliotokea misimu iliyopita ambapo bei ilishushwa hadi shilingi 300 kwa kilo na amefafanua kuwa kupitia utatatibu huo wakulima watapata malipo ya pili.

“Nataka niwahakikishie Serikali haiwezi kukubali kuona wakulima wake wananyonywa, ndio maana tumetoa fedha ili muuze kahawa yenu kupitia vyama vya ushirika, tunataka mpate fedha nzuri, lakini kama kuna wanunuzi wanaotaka kuja kununua kahawa hapa kwa bei nzuri ya shilingi 1,500 au 1,600 au hata shilingi 2,000 hatuwazuii waje kuanzia hata leo ilimradi wahakikishe wanafuata sheria na taratibu ikiwemo kulipa makato yote yanayopaswa kwa sababu baadhi ya makato hayo ni kwa ajili ya magunia na pia tunataka tuanze kutoa miche ya kahawa bure” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu tatizo la upatikanaji wa maji ambalo wananchi wa maeneo hayo wamemuomba Mhe. Rais Magufuli awasaidie kulitatua, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa ambaye yupo ziarani Mkoani Kagera kushughulikia haraka iwezekanavyo na kwa Kata ya Kyaka ametoa maelekezo kuwa wizara iwapeleke watalaamu watakaoweka miundombinu ya kuvuta maji ya Mto Kagera na kuyapandisha hadi kwenye mlima uliopigwa bomu wakati wa vita vya Kagera na kisha kuyasambaza kwa wananchi kwa mtiririko kabla ya tarehe 25 Desemba, 2019.

Katika maelekezo yake, Mhe. Prof. Mbarawa amesema wizara itatatua matatizo ya maji katika maeneo hayo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maji lakini kwa Mji wa Muleba tayari Serikali imetenga shilingi Milioni 400 na Nyakabango shilingi Milioni 600 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa hatua kubwa za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba, taasisi zinazotoa huduma za kijamii, miundombinu ya barabara na umeme, na amewasihi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuhakikisha wanadumisha amani na mshikamano ambavyo ni jambo muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote duniani.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi hao kuzitunza vizuri Hifadhi za Taifa mpya zilizoanzishwa ambazo ni Rumanyika-Karagwe, Ibanda-Kyerwa na Burigi-Chato  na pia kutumia vizuri fursa za kujipatia kipato kupitia hifadhi hizo ikiwemo kufanya biashara na watalii ikiwemo kuuza bidhaa zao za kilimo, ufugaji na nyinginezo.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha huduma za usafiri katika Ziwa Victoria ambapo meli kubwa ya abiria inajengwa na meli nyingine 5 zinakarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 152.

Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani kwenda katika Mkoa wa Kagera kushughulikia matatizo ya kukosekana kwa umeme yaliyolalamikiwa na wananchi hao.

Akiwa katika Kijiji cha Kibehe Wilayani Chato ambako wananchi wamelalamikia soko la zao la pamba, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa yote inayozalisha zao la pamba kusimamia vizuri soko la zao hilo na ameelekeza kuwa utaratibu wa kuingia mikataba na wanunuzi uwahusishe wanunuzi wengi badala ya kibali kutolewa kwa mnunuzi mmoja ili kuweka ushindani wa bei.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527