MTANZANIA ATUPWA JELA MAISHA KWA KUHUSIKA KWENYE SHAMBULIO LA KIGAIDI KENYA

Rashid Charles Mberesero, (kulia mwisho) raia wa Tanzania anayetuhumiwa kuhusika katika shambulio hilo amehukumiwa maisha gerezani

Mahakama moja mjini Nairobi imewahukumu washukiwa watatu wa ugaidi nchini Kenya waliopatikana na hatia ya kutekeleza shambulio la mwaka 2015 katika chuo kikuu cha Garissa.


Wengine wawili Hassan Edin na Mohammed Abdi jina jingine Mohamned Ali Abikar wamehukumiwa miaka 41 kila mmoja gerezani.

Wote walipatikana na hatia ya kupanga shambulio hilo chini ya ushirikiano wa wanachama wa kundi la Al-Shabab.

Takriban wanafunzi 148 walifariki katika shambulio hilo.

Kadhalika hukumu hiyo imepitishwa baada ya watatu hao kupatikana na hatia ya kuwa wanachama wa kundi la al-shabab kutoka Somalia.

Mwezi uliopita, mahakama nchini Kenya ilimuachilia huru Sahal Diriye Hussein aliyetuhumiwa kutekeleza shambulio la 2015 katika chuo kikuu cha Garissa lililosababisha vifo vya takfriban watu 150.

Awali kesi hiyo ilichelewa kuanza leo mchana baada ya wakili wa mmojawapo wa watuhumiwa Rashid Charles Mbeserero, raia wa Tanzania kushindwa kutokea mahakamani.

Hatua iliyosababisha Jaji Francis Andayi kutoa agizo kwa mawakili na kusukuma mbele kusomwa hukumu hiyo.
Rashid Charles Mberesero: ni nani?

Rashid Mberesero, aligundulika katika eneo la tukio akiwa sio mwanafunzi wala mfanyakazi wa chuo hicho.

Kulingana na gazeti la The Citizen toleo la tarehe 10 mwezi Aprili 2016, Rashid aliyesoma shule ya upili ya Bihawana mjini Dodoma alidaiwa kutoroka shule baada ya kukatazwa kuvaa kofia kichwani.

Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo wakati huo, mwanafunzi huyo alijiunga na shule hiyo mwaka 2015 baada ya kutoka shule ya upili ya Bahi Kagwe.

Chakushangaza ni kwamba licha ya kutoweka katika shule, hakuna aliyefuatilia alikokwenda

Kwa takriban miezi minne wazazi wa kijana huyo walidhani kwamba mwana wao yupo shule swala ambalo halikuwa la kweli.

Haijulikani ni nini haswa kilichomfanya kuingia katika ugaidi.

Wazazi wa Rashid walishangaa kugundua kwamba mwana wao alikuwa miongoni mwa watu waliopanga na kutekeleza shambulio la Garissa.

Waathiriwa walisubiri haki kwa muda mrefu

Kulingana na mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza waathiriwa wa shambulio hilo kama Anastasia Mikwa wanaishi na makovu ya shambulio hilo.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 kutoka chuo kikuu cha Garissa alipigwa risasi mara kadhaa wakati wa shambulio hilo.

Licha ya kufanyiwa upasuaji mara 32 bado anategemea kuangaliwa na wazazi wake.

Shambulio hilo lilitekelezwa na kundi la al-Shabab linaloshirikiana na lile la al-Qaeda katika Chuo hicho kikuu kilichopo kaskazini mashariki mwa Kenya.

Lilikuwa shambulio la pili baya zaidi katika historia ya Kenya , kufuatia shambulio la ubalozi wa Marekani nchini Kenya la 1988 ambapo zaidi ya watu 200 waliuawa.

Kwa kuwashambulia vijana na wataalam wa siku zijazo shambulio hilo lililenga kuathiri ukuaji wa uchumi na uthabiti wa taifa mbali na kuleta mgawanyiko wa kidini.

Wapiganaji wanne waliotekeleza shambulio hilo waliuawa katika eneo la mkasa huo huku mtu aliyepanga Mohammed Kuno akiuawa katika shambulio nchini Somalia 2016.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post