TPDC YAONGEZA MTEJA MPYA WA VIWANDANI

Meneja wa Biashara za Gesi, Mhandisi Dora Ernest (kulia) akimpatia mkataba wa makubaliano kwa Mkurugenzi wa Shreeji Silicates Tz Ltd, Bw. Mukkasa Giridhar Rao (kushoto)  ambapo amesema kutumia gesi asilia wataweza kuokoa asilimia 30% ya gharama za uzalishaji ambazo wamekuwa wakitumia sasa.
---

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) leo hii limetia saini mkataba wa mauziano ya gesi asilia na kampuni ya Shreeji Silicate Tz Ltd. Makubaliano hayo yanaiwezesha TPDC kuuza gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 0.4408 kwa siku kwa kipindi cha miaka miwili ambapo kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeaka hadi kufikia futi za ujazo milioni 0.9 kwa siku.

Akiongea baada ya kutia saini mkataba huo Meneja wa Biashara za Gesi, Mhandisi Dora Ernest alisema “mkataba huu utatuwezesha kusambaza gesi asilia kwa Shreeji Silicates kwa kipindi cha miaka 10 ambayo inaweza kuongezeka kutokana na makubaliano yalivyo”. Mhandisi Dora anasema mteja huyu anakuwa mteja wa 45 wa viwandani ambapo kiwanda chake kiko eneo la Mkuranga na anachukua gesi asilia kutoka katika bomba linalosambaza gesi kwa kiwanda cha vigae kilichopo Mkuranga ambacho kimechukua gesi kutoka kituo cha valvu namba 12 (BVS 12) kilichopo Njopeka, Mkuranga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shreeji Silicates Tz Ltd, Ndg. Mukkasa Giridhar Rao anasema “kwa kutumia gesi asilia tuna uhakika wa kuokoa asilimia 30% ya gharama za uzalishaji zinazotokana na nishati kitu ambacho kitatuongezea ufanisi kama kiwanda”. Ndg. Rao anaeleza kwamba kampuni yake inajishughulisha na uzalishaji wa kemikali za sodium silicates ambazo hutumika kuzalisha bidhaa za sabuni za aina mbalimbali.

Matumizi ya gesi asilia ni nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati na TPDC kama kampuni ya Taifa ya Mafuta ndio yenye jukumu la kusambaza nishati hiyo kwa wateja kama vile wa kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na hata kwenye magari. Katika kuteleza majukumu haya, TPDC inatumia kampuni tanzu ya GASCO. Matumizi ya gesi asilia vile vile ni rafiki wa mazingira hivyo wenye viwanda pamoja na wananchi wa kawaida wanahimizwa kutumia rasilimali hii ili kulinda mazingira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527