NAIBU KATIBU MKUU(E) OR-TAMISEMI : ANDAENI VIPINDI VINAVYOELEZEA MAFANIKIO YA ELIMU KATIKA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Naibu Katibu Mkuu(E) OR-TAMISEMI Bw. Tixon Nzunda amewataka maafisa habari na mawasiliano ya Umma,  wanahabari na waandaaji wa maudhui ya katika mikoa inayotekeleza program ya EQUIP-T 2014-2019 kuandaa maudhui ya vipindi yanayoelezea mafanikio ya sekta ya elimu ya awali na msingi yaliyofanywa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.


Hayo aliyasema Jana Julai 29, 2019 wakati akifungua kikao cha siku tatu(3) chenye lengo la  kuwakutanisha wadau wa mbalimbali wa elimu katika kujadili kwa kina juu ya kazi zinazofanyika kwenye sekta ya elimu(Awali,  Msingi,  Mazingira,  Mafanikio)  pamoja na namna walivyopokea njia mbadala za kuwawezesha watoto kujifunza na kujenga mazingira bora ya kujifunzia. 

Alisema kuna mambo mengi sana ambayo yamefanywa na Serikali katika uboreshaji wa elimu ya Awali na msingi,  ikiwemo kuondolewa kwa Ada za kujiunga na masomo,  ujenzi wa mindombinu mambo ambayo wananchi hawajaelezwa kwa undani zaidi na hivyo wananchi hawajui kama yamefanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wengine. 

“Utendaji wa walimu umeboreshwa,  vyumba vya madarasa vimeongezeka kwa 91%,  uanzishwaji wa vituo vya vituo 3,059, ujenzi wa matundu ya vyoo na ongezeko la uandikishaji wanafunzi kuongezeka haya ni baadhi ya mafanikio” alisema Bw.  Tixon. 

Mbali na hilo amepiga marufuku walimu wa shule za awali na msingi kuanzia Darasa la kwanza hadi la Tatu,  kuingia darasani na viboko akisema viboko vinamtengenezea mtoto mazingira  uoga katika kujifunza. 

“Kuanzia leo napiga Marufuku kwa walimu wote nchini kuanzia elimu ya awali na msingi mpaka darasa la tatu(3) walimu kuingia madarasani wakiwa wamebeba fimbo,  kama ni zana za kufunzia watafute vitu vingine na sio viboko” alisema

Kwa miaka kadhaa iliyopita sekta ya elimu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya baadhi ya wanafunzi kumaliza Elimu ya Msingi bila kujua kusoma,  kuandika na kuhesabu(KKK). 

Hii ilipelekea ofisi ya Rais-TAMISEMI kuanzisha na kutekeleza programu mbalimbali zenye lengo la kuimarisha ujifunzaji wa stadi za KKK hasa kwa wanafunzi wa darasa la Kwanza na darasa la pili. 

Programu ya kuinua ubora wa elimu elimu nchini(EQUIP-T)  ni ya miaka 6 iliyoanza kutelekezwa  mwaka 2014 na itafika ukomo Januari mwaka 2020.

Programu hii inafadhiliwa kwa msaada wa ruzuku ya Paundi milioni 37.2 kutoka serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo ya Kimataifa-DflD. 

Malengo ya Program ya EQUIP-T ni kuinua ubora wa elimu nchini kwa kuongeza matokeo ya ujifunzaji wa mwanafunzi kwa darasa la Kwanza na la pili hasa kwa wasichana kwenye Mikoa 9( Halmashauri 63 na shule 5,196) ambayo ndiyo iliyoshiriki kikao hicho iliyoonekana ina kiwango cha chini cha ujifunzaji  ambayo ni Dodoma,  Katavi,  Kigoma,  Lindi,  Mtwara,  Mara,  Shinyanga,  Simiyu,  Singida na Tabora. 

Kikao hicho kimewashirikisha Maafisa elimu kata,  watendaji wa EQUIP-T,  Wakuu wa shule,  walimu wa shule za awali na Msingi,    wanahabari,  maafisa mawasiliano ya umma na OR-TAMISEMI.

Naibu Katibu Mkuu (E)  OR-TAMISEMI Tixon Nzunda akizungumza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527