SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 1 KUTOKA BENKI YA POSTA TANZANIA (TPB)

Na Saidina Msangi na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imepokea gawio la Shilingi Bilioni 1 kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB) linalotokana na faida ya uwekezaji wake wa asilimia 83 ya hisa  katika Benki hiyo katika mwaka wa fedha 2018/19.


Hafla ya makabidhiano ya Hundi kifani ya gawio hilo imefanyika jijini Dodoma, kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ambaye alipokea kwa niaba ya Serikali, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo Dkt. Edmund Mndolwa.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mpango aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

“Utoaji huu wa gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki inazidi kukua na kuwapa moyo watanzania na wawekezaji kuwa TPB inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Mpango.

Aliitaka Benki hiyo kuongeza wigo wa utoaji huduma ili kuwafikia wananchi hususani waishio vijijini pamoja na kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusu umuhimu wa  kuweka akiba, kukopa sambamba na kurejesha mikopo kwa wakati.

“Riba katika benki zetu bado ni kubwa taasisi za fedha zione namna ya kuzipunguza sambamba na kutoa mikopo kwa kuzingatia kanzidata ya wakopaji ili kuepuka mikopo chechefu.”, alisisitiza Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango ameiagiza Benki hiyo kuendelea kuwapa wanawake  kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo ili waweze kuendesha shughuli za maendeleo.

Pia Dkt. Mpango aliiagiza  TPB kusimamia uadilifu kwa watumishi wake na kuwa makini na kutoa taarifa za  miamala yenye mashaka ili kuzuia utakasishaji wa fedha haramu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPB Dkt. Edmund Mndolwa alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh. Bilioni 17.2 kabla ya kodi ambayo Benki yake imeipata katika mwaka wa fedha 2018/19. Pia ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Mndolwa aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa utendaji mzuri ambao umeiwezesha Benki hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527