Rais Magufuli Atoa Neno Kwa Watanzania Kuhusu Uchaguzi Wa Serikali za Mitaa.....IGP Sirro Kasema Jeshi la Polisi Liko Imara Kulinda Uchaguzi Huo

Rais Magufuli amewataka Watanzania kutumia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka 2019 kuwachagua viongozi wazuri na sio watoa rushwa.

Magufuli ametoa wito huo leo Jumatatu Julai 15,2019 wakati akizungumza na wananchi wa Katoro na Buselesele mkoani Geita akiwa njiani kuelekea Magogo Geita ambako atazindua nyumba za askari wa jeshi la polisi.

“Mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa, chagueni viongozi wazuri, msichague viongozi wanaowapa rushwa, mkikosea kuchagua madhara yake ni makubwa.”

“Mkasimame imara katika kuchagua viongozi ambao mnafikiri wataweza kunisaidia pia na kunishauri vizuri,” amesema

Rais Magufuli pia amesisitiza wakazi wa maeneo hayo kudumisha amani, upendo na umoja na kutokubali kufarakanishwa.

 
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini  IGP Simon Sirro amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa vikosi vyake vimejipanga kuhakikisha amani na utulivu vitatawala katika chaguzi zijazo.

Amesema viongozi wazuri watachaguliwa kukiwa na Amani na utulivu hivyo watahakikisha hali hiyo inatamalaki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Nakuhakikishia amani itatamalaki na uchaguzi utapita salama. Hatutamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga amani. Sisi vyombo vya dola tuko tutahakikisha tunafuata sheria kuhakikisha wananchi wanaishi salama,” amesema


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments