PROFESA ANNA TIBAIJUKA ATANGAZA KUNG'ATUKA UBUNGE

Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), amesema hatagombea tena nafasi ya ubunge Uchaguzi Mkuu ujao. Tibaijuka  alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na  Ayo Tv


Pamoja na mambo mengine, alisema anastaafu kwa sababu yeye ni kizazi cha Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliwafundisha kung’atuka.

“Mimi 2020 ninastaafu, ninang’atuka kwa sababu sisi ni kizazi cha Mwalimu Nyerere na katika vitu alivyotufundisha ni kung’atuka.

“Katika uchaguzi wa 2015, Muleba Kusini pamoja na kampeni ya Escrow bado nilipita kidedea, kwa kweli nawashukuru wananchi wa Muleba, ni watu wanaotafuta maendeleo, wana kiu ya maendeleo.

“Na ninaposema nastaafu ubunge, haimaanishi kwamba nastaafu Muleba, hivi ni vitu viwili tofauti, mimi ninastaafu uwakilishi, Bunge letu hili lingekuwa Seneti ningesema nitaendelea.

“Lakini sasa ni Bunge la Uwakilishi, hatuna Bunge la Seneti, yaani Bunge ambalo sasa hoja zinalinda masilahi mapana ya umma, hapa tunawakilisha wananchi na mimi naamini tunaweza kupata mwakilishi mzuri wa Muleba,” alisema.

Alisema anaamua kung’atuka si kwa sababu ya kuhofia kushindwa, kwani ingekuwa hivyo angeshindwa katika uchaguzi uliopita kutokana na kampeni chafu juu yake.

“Mimi kama kupigwa chini, ningepigwa chini mwaka 2015 au sio. Asiyekubali kushindwa si mshindani, kwa hiyo mimi sistaafu kwa ajili ya hofu, kwanza Muleba anayenishinda ni nani? Ni Mwenyezi Mungu peke yake.

“Kwa kipindi cha miaka 10 nimejifunza, nimeelewa matatizo ya wananchi na wakati ule nilipotoka Umoja wa Mataifa, nilikuja na nia moja ya kujifunza kwamba taifa letu lina tatizo gani.

“Tufanye nini ili tuweze kusogea mbele, kwa hiyo hata bungeni ninaposimama, nikiona kitu hakijakaa sawa huwa sisimami kiitikadi, pia sitaki ushabiki ambao hauna mantiki,” alisema.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527