MKUU WA WILAYA YA IKUNGI, MIRAJI MTATURU ASHINDA KURA ZA MAONI CCM KUMRITHI TUNDU LISSU


Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Singida Mashariki, wamepiga kura kupata mwana CCM mmoja ambaye atapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Julai 31.

Katika mkutano huo uliofanyika jana, wanachama 13 walichuana katika uchaguzi huo na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu, ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 396.


Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kupoteza sifa za kuwa mwakilishi wa wananchi kwa kushindwa kutoa taarifa za mahali alipo pamoja na kutojaza fomu za mali na madeni.

Kutokana na hatua hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Julai 5, ilitangaza ratiba ya uchaguzi huo.

Mbali ya Mtaturu, wana-CCM wengine waliochuana katika kura hizo za maoni ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni mstaafu Chiku Galawa aliyepata kura 40.

Wengine na kura zao katika nabano ni Thomasi Kitima (79), Martini Lissu (29), Lazaro Msaru (17), Hamisi Maulidi (12),  Mwanahamisi Mujori (7), Mariamu Nkumbi (7), Moris Mukhoty (4), Jeremia Ihonde (4), Sylivester Meda (3), Shilinde Kasure (1) na Emmanuel Hume (1).

Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na utulivu, kila mgombea aliweza kunadi sera zake mbele ya wapigakura na kisha kuulizwa maswali kwa mujibu wa utaratibu uliotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu wa Sekreterieti CCM Taifa, Salum Leja.

Leja alisema kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wamekamilisha kazi yao ya hatua ya kwanza na sasa kinachofuata majina ya wagombea watatu yatakwenda katika vikao vya ngazi ya juu ya chama..


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527