MEMBE ASHANGAA TUNDU LISSU KUVULIWA UBUNGE.... AZUNGUMZIA MATUKIO YA UTEKAJI NCHINI


Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amewataka viongozi wa dini, serikali na wastaafu kukemea suala la utekaji kwani haiwezekani watu kuishi nchini kwa wasiwasi.


Amezungumza hayo leo  na waandishi wa habari katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam  wakati alipokuja kusikiliza kesi ya madai aliyofungua dhidi ya mmiliki wa gazeti la Tanzanite, Cyprian Musiba na wachapishaji wa gazeti hilo.
 

“Huu ni utamaduni mpya ambao haukubaliki na ningependa kuchukua nafasi hii kusema kwamba suala la utekaji na watu kupotea linaweza kuiondolea nchi yetu heshima duniani tangu tupate uhuru, hivyo ningependa kuwaomba viongozi wote walikemee,”

“Viongozi wa serikali wasione aibu hata wa Dini wasiogope na wastaafu wote lazima tukemee utamaduni huu mpya, hatuwezi kuendelea kuishi katika nchi yenye watu wenye wasiwasi na uoga ambao hawajui kesho wataamka vipi na hii ajenda iishe maana isipo isha itaenda kwenye uchaguzi mwakani,” Membe

Aidha, akizungumzia kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kupoteza ubunge, Membe amesema kama Mtanzania ameshangaa sana.

“Mimi kama Mtanzania  nilishangazwa sana na uamuzi wa Spika, Job Ndugai lakini tusubiri Lissu arudi.

“Nina uhakika atakwenda mahakamani kudai haki yake na kama ipo haki ataipata mahakamani,” amesema Membe


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527