MANGULA ATOA ONYO KWA WANACHAMA WA CCM WALIOANZA KUUSAKA UBUNGE, UDIWANI


Makamu  Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, ameonya wanachama wa chama hicho wanaojipenyeza kuwania ubunge na udiwani wakati viti hivyo bado vina watu.

Alitoa onyo hilo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa mkutano kuwapongeza wanaCCM wa Jimbo la Singida Mashariki kbaada ya Miraji Mtaturu kutangazwa kuwa mbunge akimrithi Tundu Lissu.

“Natoa maelekezo kuwa mtu yeyote atakayebainika kuanza kujipenyeza kwenye majimbo kuanza kufanya kampeni ya kuwania nafasi hizo za uongozi hatutamwonea huruma, tunamchukulia hatua za kinidhamu,” alisema Mangula.

Alisema katika majimbo kuna wawakilishi ambao muda wao wa miaka mitano bado haujaisha, hivyo waachwe watekeleze ilani ya chama hicho kwa kuwapelekea wananchi maendeleo.

Alisema mwanaCCM mwenye nia ya kutaka nafasi hizo, anatakiwa kusubiri muda utakapofika na wanachotakiwa sasa ni kwenda kwa wananchi kutangaza kazi za maendeleo zilizofanywa na viongozi waliopo madarakani.

Alitoa maagizo kwa wanaCCM kuwa pindi watakapomwona mtu yeyote ameanza kujipenyeza katika majimbo hayo, watoe taarifa ili aweze kuchukuliwa hatua kupitia kamati ya maadili.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527