LUGOLA AAGIZA POLISI KUWASAKA WANAOTOA TAARIFA ZA UONGO KUTEKWA, KUPOTEA KWA WATU NCHINI


Na Mwandishi Wetu, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafunguliwa mashtaka wanaosambaza taarifa za uongo, ambazo zinatengenezwa kuhusu matukio ya utekaji na kupotea watu wakiwa na lengo la kuichafua taswira ya Serikali.


Lugola amesema baadhi ya watu hao ambao wana nia mbaya ya nchi,  wanakaa mitandaoni kuanzia asubuhi hadi jioni wakizusha matukio hayo machafu wakiwa na lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa kwa kuichonganisha Serikali Rais Dkt. John Magufuli na wananchi wake, ambayo inaendelea kufanya kazi nzuri kwa kuiletea nchi maendeleo kwa kasi zaidi.


Waziri Lugola ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipokuwa anajibu maswali mbalimbali ya wananchi wa Mji Mdogo wa Kisorya, Kata ya Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo mmoja wa wananchi hao alimuuliza Waziri huyo kuhusu Wizara yake imejipangaje kuyasambaratisha matukio ya utekaji, kupotea watu hususani tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari.


“Lazima tuwe na uchungu na taifa hili, taarifa hizi zinazoripotiwa na watu kupotea ama kutekwa zipo katika makundi mawili, moja ni taarifa za uongo, za kutengeneza, wakiwa na lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa, wakiropoka hovyo, na miongoni mwa watu hao wanaodaiwa kutekwa ama kupotea, wengine tumewabaini wanajiteka wenyewe, wanajipoteza wenyewe, na kuna wengine wameshafikishwa mahakamani kwa kutoa taarifa za uongo kuwa wametekwa, au kupotea,” alisema Lugola na kuongeza;
“Siku hizi kupitia mitandao ya kijamii, kuna watu wanatunga matukio ya uongo, wanatengeneza matukio ya kutekwa na kupotea, ndugu zangu Watanzania, taarifa hizi zinaweza kuigawa taifa, kusababisha machafuko na kusababisha taharuki katika jamii.”


Lugola pia amesema, kuna baadhi ya taarifa za kweli na Serikali inakubali yapo matukio ya mtu kuweza kupotea au kutekwa, na hata kutoonekana katika familia yake, hiyo haipingwi na Serikali inakubali yapo, lakini pia wapo ambao wanakua kweli wamepotea ama kutekwa, serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama hususani Jeshi la Polisi, limekua likiendelea kuwatafuta watu hao, na wakati linapoendelea kuwatafuta Jeshi linahitaji pia taarifa za wananchi kuwezesha kuwapata watu hao.


“Ndugu wananchi, pia kuna taarifa za upotoshaji kwa watu wanaodaiwa kupotea au kutekwa kweli, lakini wengine wanasambaza taarifa za uongo, tumekuwa tukishuhudia katika baadhi ya migodi ya madini, wakitatafuta utajiri, lakini majumbani kwao walishafanya mpaka matanga wakiamini ndugu yao alishafiriki kwa kutekwa au kupotea, kumbe anatafuta utajiri machimboni,” alisema Lugola.


Alisema Serikali yoyote duniani ambayo imechukua dhamana ya kuwalinda wananchi wake halafu Serikali hiyo hiyo igeuke kuwateka na kuwaua, Serikali ya namna hiyo haipo duniani.


“Naelekeza Jeshi la Polisi, kwa wale ambao wanatunga maneno ya uongo na kuchonganisha Serikali na wananchi, muwasake popote walipo, muwakamate na muwafikishe katika vyombo vya sheria,” alisema Lugola.


Lugola alijibu swali hilo la kuhusu utekaji na upoteaji wa watu baada ya Mkazi wa Kisorya, Mnyaga Semba alipokuwa anataka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na matukio hayo.


“Mbunge wangu, wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, nataka nijue kundi linaloteka watu, kushambulia watu,  na pia jambo hili tena limezuka juzi Waziri wetu wa Mambo ya Nje alipokuwa anahojiwa tukasikia jambo la mwandishi wa habari, Azory mara kazikwa mara hivi, naomba kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na jambo hili?,” alisema Semba.


Aidha, Lugola alizungumzia kuhusu uhalifu katika ziwa Victoria, ambapo wananchi wananyang’anywa mashine, nyavu na samaki na wahalifu hao, kuwasababnishia wananchi umaskini, alilitaka Jeshi la Polisi kuwasaka wahalifu hao kwa kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo ya ziwa kwa lengo la kudhibiti uhalifu huo.


Pia Waziri huyo, alilitaka Jeshi hilo kutowasumbua waendesha bodaboda kwa kuwakamata hovyo barabarani na bodaboda hizo kuzihifadhi vituo vya polisi huku wamiliki wa vyombo hivyo wakiteseka kuzipata.


“Bodaboda akifanya makosa mpigeni faini, na apewe muda wa siku saba kulipa faini hiyo kama inavyokua katika faini za magari. Na nilishasema, bodaboda ambazo zinapaswa kuwepo kituoni ni za aina tatu tuu, ambazo zilizoshiriki uhalifu, zilizookotwa na zilizopata ajali, ndizo nilizoagiza ziwepo kituoni,” alisema Lugola.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post