KATIBU MKUU JUMUIYA YA MADOLA AFANYA MAZUNGUMZO NA PROF. KABUDI – LONDON,UINGEREZA


Jumuiya ya Madola imeonesha kuridhishwa na namna Tanzania inavyotekeleza mageuzi ya kiuchumi,uwajibikaji na uawala bora kwa wananchi wake jambo ambalo jumuiya hiyo inalihimiza na kulisimamia kwa Nchi wanachama wake.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi za sekretarieti ya jumuiya hiyo zilizopo London Nchini Uingereza.

Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland ameeleza kuridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Prof. Palamagamba John Kabudi kuhusu utekelezaji wa masuala ya demokrasia,utawala bora na utawala wa sheria pamoja na Haki za binadamu nchini Tanzania na kwamba Jumuiya hiyo inatambua  juhudi hizo na inaunga mkono hatua hiyo.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa mbali na kuhimiza utekelezaji wa utawala bora,haki za binadamu na utawala wa sheria pia Jumuiya ya Madola imelenga kukuza na kuwezesha biashara miongoni mwa nchi wanachama ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo kupitia shirika la biashara la kimataifa (WTO) na mashirikiano ya biashara ya kikanda.

Amesema ni jukumu la nchi za Jumuiya ya Madola kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu katika jumuiya hiyo ili kuiwezesha kupiga hatua za haraka za kimaendeleo na kuifanya  Jumuiya nzima kuendelea bila ya kuacha nchi nyingine nyuma kutokana na uwepo wa migogoro ama machafuko ya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa wanachama wa Jumuiya. Katika hili ameisifia Tanzania kwa kuwa na Amani na utulivu muda wote na pia kushiriki katika juhudi za kutatua migogoro kwa nchi zingine wanachama na wasio wanachama wa Jumuiya.

Kuhusu suala la mabadiliko ya tabia nchi,Katibu Mkuu huyo wa jumuia ya madola amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi. Ameeleza kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika program mbalimbali zinazolenga kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na masuala ya mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. palamagamba John Kabudi amemhakikishia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuwa Tanzania inaipa umuhimu mkubwa jumuiya hiyo na itaendelea kushirikiana nayo katika masuala ya ukuzaji wa uchumi, utawala bora hususani wakati huu ambapo Tanzania inafanya mageuzi ya kiuchumi katika kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Ameipongeza  jumuiya ya madola  kwa mpango maalum inayoandaa kwa ajili ya kukuza na kuongeza  biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo kwa ujumla jambo ambalo litafungua fursa biashara na masoko kwa bidhaa na mazao ya Tanzania. Amemuahidi Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania itashiriki ipasavyo katika mpango huo.

Katika mazungumzo hayo,  Waziri Kabudi pia amekubaliana na Bi Scotland kuangalia namna ya kuwasaidia vijana kuongeza ubunifu ili waweze kujiajiri na kuimarisha uchumi ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana huku akimpongeza Katibu Mkuu huyo kwa mageuzi makubwa anayoyafanya ndani ya jumuiya hiyo ili iweze kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi zaidi.

Profesa Palamagamba John Kabudi yuko London Nchini Uingereza kwa ziara ya siku nne kuhudhuria mkutano wa Mawaziri wa mambo ya Nje wa Jumuiya ya madola pamoja na mkutano wa Kimataifa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post