KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI NCHINI LIMESAIDIA KUWEKA MAZINGIRA SAFI


Na Faidha Jumanne-Maelezo.
Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya mazingira imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa mifuko bora mbadala kwa wananchi. 


Hii imetokama na jitihada za serikali za kupiga marufuku mifuko hiyo, kuanzia tarehe 01 Juni 2019 na kupelekea kupatikana kwa mifuko mbadala,  kwa wananchi inayoimarisha afya zao kuongeza ajira na kupunguza uchafuzi wa mazingira. 


Akihojiwa na Idara ya Habari - MAELEZO, Afisa Habari Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Lulu Musa, alianza kusifia juhudi zilizopatikana kwa muda mfupi, huku akirejea Siku ya Maazimisho ya Usafi Kitaifa Jijini Dodoma, yaliyofanyika Juni 5, 2019. 


``Tumetoa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa wananchi, kazi hii inafanywa na Halmashauri za Serikali za Mitaa- TAMISEMI kwa kusimamia maeneo yao kwa kutotumia mifuko ya plastiki hakika wanastahili pongezi, nasema hongereni sana”. 


Uamuzi wa Serikali kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki lengo lake ni kuboresha usafi wa mazingira na kuwaweka wananchi katika hali ya kuepuka magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara damu. 


“Lengo ni kuimarisha afya.  Kadhalika, mazingira salama ambapo, sote tunatambua umuhimu wa mtu kuwa na mazingira mazuri na yenye usalama kiafya kwa kushiriki katika shughuli za kijamii na za kitaifa”. Amesisitiza Lulu. 


Ameongeza  serikali itaendelea kuwa macho kufuatilia mwitikio mzuri wa wananchi kutoendelea kutumia mifuko ya plastiki, na kutotegemea watu wengine kusimamia mazingira ya Watanzania, kadhalika akasema bali iwe ni zoezi la kawaida kwa wananchi.  


Lulu akazidi kufafanua kuwa, serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutunza mazingira kwa lengo  la kuboresha afya zao na kufahamu kwa kina mifuko ya plastiki kwa kiasi gani imeleta madhara na kusababisha magonjwa ya aina mbalimbali yakiwemo nyemelezi,  kuteketeza uhai wa viumbe kama vile samaki na mifugo. 


Aidha, Tanzania ni nchi miongoni mwa nchi zilizoonekana katika orodha ya matumii makubwa ya mifuko uya plastiki. Hii ilitokana na kuongezeka kwa kasi kwa matumizi hayo kadiri siku zilivyozidi kwenda, amesema Lulu.  


Imeelezwa pia, Serikali kwa kushilikiana na wadau kama Shirika la Viwango Tanzania -TBS limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwenye sekta ya afya na mazingira yenye lengo la kuboresha matumizi ya mifuko mbadala na kuimalisha afya za wananchi. 


Mfano, TBS imeweka viwango vya ujazo kwenye mifuko ya plastiki ambayo bado inatumika kama vifungashio kuepusha kuzagaa kwa mifuko ya plastiki na kusababisha uchafuzi wa mazingira. Pia, imebainisha  viwango vya mifuko ambayo imeruhusiwa kwa kutumika kwa kufungashia chakula pamoja na madawa ya kilimo kwa kuangalia uzito/ujazo wa bidhaa, aina za bidhaa ambazo zitatumia mifuko hiyo ili kuweza kusaidia katika utunzaji wa mazingira. 


Vilevile,  Lulu aliongezea kuwa shirika la viwango, TBS litakua na uwezo wa kuwasiliana na wananchi kwa njia yoyote ile hata ikiwa kimtandao kwa kuwapa taarifa ya matumizi ya mifuko iliyo bora na yenye viwango  ili kuweza kusaidia kutoa huduma bora kwa wanainchi. 


Akielezea mfumo wa matumizi ya kidigitali Lulu amesema kuwa, Tanzania ilishaingia mfumo wa matumizi ya kidigitali katika utoaji huduma kwenye maeneo mengi, na imekuwa msaada mkubwa katika shirika la viwango TBS. 


Hata hivyo Tanzania imekua na matumizi mazuri ya mfumo wa kidigitali kwa kutoa mawasiliano kwa wananchi katika mambo mbalimbali ya kijamii na kuleta mafanikio chanya katika mwitikio wa jambo kama hili la katazo ya mifuko ya pllastiki, Lulu akasema, “Kupitia mfumo huu wa kutoa mawasiliano katika mitandao ya kijamii utasaidia kuongeza uwingi wa watu katika kupata taarifa kwa uharaka na sisi kutupelekea ufanyaji kazi wetu kutoa taarifa haraka kwa umma”.
`` … tutaendelea kuwa na utaalamu wa hali ya juu kwa kuhakikisha taarifa tutakazo zitoa zitakuwa taarifa sahihi zenye viwango sahihi kwa kutoa msaada mkubwa sana kwa kuwa hizi taarifa ni za muhimu sana kwa wananchi’’.   


Akiongea mmoja wa wananchi waliohojiwa,  Hashim Chikwaya ambaye ni mkulima amesema, “  Kutokana na kusitishwa  kwa mifuko ya plasiki,  hakika hili ni jambo jema sana kwa wananchi kwa kuwa wananchi walikuwa wakitumia mifuko hiyo kwa kuhifadhia chakula ambacho chakula hicho ni chenye joto” alisema Chikwaya.  


Akaendelea Chikwaya ambaye anaonekana kuwa na uzoefu wa kujua athari za mifuko, kuwa Kutokana na joto la kwenye mfuko linasababisha kutoa mvuke wenye majimaji ya tindikali ambayo imetumika kutengenezea mfuko huo na kuingia kwenye chakula, iwapo chakula hicho kikiliwa na mtu, hupata athari kubwa za kiafya.   


Vilevile, akielezea zaidi adhari za kiafya Chikwaya alisema “Kulikuwa na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima pale mtu anapochukua mfuko wa plastiki kwa matumizi ya kuwashia moto, hususani jiko la mkaa, kitendo hicho kinapofanyika mtu huyo anavuta hewa ya mfuko unaoyeyuka na kumsababishia madhara ya kupata ugonjwa wa kansa”. 


Akimalizia, Chikwaya alisema, mbali na uchafuzi wa mazingira mara nyingi, mfano hospitali madaktari walikuwa wakishauri kuepukana na matumizi ya vifaa vya plastiki kuhifadhia chakula chenye joto na kusema kuwa plastiki hizo huchubuka zipatapo joto na kusababisha athari ya upatikanaji wa magojwa pinde ulapo chakula hicho, akaongeza, “hata hivyo si rahisi kuona michubuko hiyo kwa macho”.  


Zoezi la katazo la Mifuko ya Plastiki limeanza Juni mosi, 2019 ambapo mpaka sasa kwa tafiti imeonyesha mafanikio, mfano katika Jiji la Dar-es-salaam wengi waliohojiwa mitaa ya Kariakoo wamesema mitaa yao inaonekana safi kwa kuondolewa mifuko hiyo na hivyo wanaishukulu serikali.      


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527