CHAMA CHA TLP CHAMTEUA RAIS MAGUFULI KUWA MGOMBEA WA URAIS 2020


Mwenyekiti wa Chama Cha TLP, Augustine Mrema amesema kuwa chama chake kimefikia uamuzi kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 hususan nafasi ya urais na wameamua kuwa ‘mgombea wao’ atakuwa Rais John Magufuli.

Mrema ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, amesema kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho ilifikia uamuzi huo hivi karibuni.

Ameeleza kuwa baada ya kutathmini kazi aliyoifanya Rais Magufuli, wameona hakuna haja ya kuweka mgombea mwingine wa urais katika uchaguzi huo bali wamuunge mkono.

“Tulitafakari kwa makini kazi anayoifanya Rais wetu… anafanya mambo makubwa ambayo yamewahi kutendeka ndani ya nchi yetu ukiondoa utawala wa Mwalimu Nyerere ambaye ametuletea uhuru,” alisema Mrema.

“Tukaangalia Rais huyu pia anajaribu kupaisha uchumi wa nchi ulingane na dunia ya kisasa, ametengeneza Reli ya Kisasa, anatengeneza Bwawa la Kuzalisha Umeme Rufiji. Tuliona kwanini tushindane naye, kwanini tupoteze rasilimali za nchi… sisi tukasema tutamuunga mkono Dkt. John Pombe Magufuli, hatutaweka mgombea na tukataka iwe ni message (ujumbe) hata kwa wanasiasa wengine ambao amedai hawana fadhila,” aliongeza.

Aidha, Mwanasiasa huyo mkongwe alieleza kuwa atagombea tena Ubunge wa jimbo la Vunjo na anaamini ataungwa mkono na Rais Magufuli. 

Amesema anarudi kugombea katika jimbo hilo ambalo aliwahi kuwa mbunge wake kwakuwa ameambiwa na wananchi kuwa wanamhitaji tena.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527