SERIKALI YAKABIDHI MFUMO WA USIMAMIZI WA MASHAURI OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI


Na.Paschal Dotto-MAELEZO.
 Serikali Kupitia Wakala ya Mtandao (e GA) imekabidhi rasmi Mfumo wa Taarifa wa Usimamizi Mashauri, kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ili kuiwezesha Ofisi hiyo Kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi Mkubwa. 


Akizungumza ya Waandishi wa Habari katika makabidhiano kati ya Wakala ya Serikali ya Mtandao na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali, Injinia, Benedict Ndomba, amesema kuwa Ofisi yake inatumia wataalam wake wa TEHAMA kutengeneza mifumo inayorahisisha kufanya kazi katika Taasisi mbalimbali nchini. 


Injinia Ndomba, alisema kuwa serikali ya Awamu ya Tano inalo kusudi kubwa la kutekeleza ahadi zake kama utoaji huduma nzuri kwa wananchi ikiwemo hiyo ya utengenezaji mifumo ya huduma kwa ajili ya kero za wananchi. 


“Serikali hii ya Awamu ya Tano, ina hazina kubwa ya wataalam wa TEHAMA, ambapo kielelezo kimojawapo ni kuwa mfumo huu umebuniwa, umesanifiwa na kutengenezwa na Watumishi wa Umma na tumekubaliana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa Mfumo huu utekelezwe kwa awamu mbili ili kuweza kukidhi mahitaji ya wadau wote”, Injinia Ndomba alisema. 


Katika awamu ya Kwanza ya Utengenezaji Mfumo huo, Ndomba alisema wametengeneza Moduli itakayoisaidia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yao hasa ya ndani kwenye masuala ya Usimamizi Mashauri, ambapo pia itakuwa ni nyenzo muhimu wa utekelezaji majukumu kwa haraka. 


Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Clement Mashamba  ameipongeza Wakala ya Mtandao wa Serikali (e GA) kwa kutengeneza mfumo huo kwa mahitaji ya ofisi ya Wakili wa Serikali na kudai kuwa watakuwa wanatekeleza majukumu kwa haraka na kwa ufanisi zaidi katika kutatua kero za wananchi. 


“Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na Wakala ya Serikali ya Mtandao ili kuhakikisha awamu zote za utengenezaji wa mfumo huu zinatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaostahili, lakini pia Ofisi yangu inatambua Mchango huu mkubwa kwa kazi zetu ya kisheria,” Dkt. Mashamba. 


Aidha Dkt. Mashamba alisema kuwa mfumo huo utakuwa ni muhimu katika kutatua kero za wananchi, hususani Usimamizi wa majalada ya Mashauri; Usajili wa Mashauri; Upangaji wa Mashauri yanayoshughulikiwa; Ufutiliaji wa Maendeleo ya Mashauri; Huduma zingine ni Usimamizi wa Ratiba ya Mashauri; Utoaji wa Taarifa; Uhakiki wa Mwenendo wa Mashauri na Uhamishaji wa Taarifa na Takwimu. 


Dkt. Mashamba alieleza kuwa mfumo huo una umuhimu mkubwa kwani unaweza kutumiwa na idara mbalimbali za Serikali na unapatikana mahali pamoja kwa hiyo ni mfumo ambao Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. 


Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post