MABADILIKO YA TABIA YA NCHI YAONGEZA KASI YA UKATILI MKOANI NJOMBE

Na Amiri kilagalila-Njombe

Vipigo katika familia na ukatili wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya wanaume dhidi ya watoto na wake zao mkoani Njombe umetajwa kusababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha akina mama kutembea mwendo mrefu kwenda kuteka maji pamoja na kuokota kuni.

Mabadiliko hayo ya tabia nchi pia yametajwa kuwa chanzo cha watoto na wanawake kubakwa pindi wanapo kuwa porini kwenye shughuli za kijamii ambako kumekuwa kikwazo kikubwa katika ustawi wa jamii.

Kwa kuona hilo shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya ushirikishwaji wa jamii katika miradi endelevu la community participatory in sustainable development organization[COPASDO] lililopo nazareth mjini Njombe chini ya ufadhili wa mfuko wa wanawake[Women Fund Tanzania] limelazimika kuanza kutoa elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuepukana na ukatili dhidi ya wanawake,wasichana na watoto kwa kuanza na kata ya yakobi ndani ya halmashauri ya mji wa Njombe.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Nestory Mahenge anasema  ili kukabiliana na vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wanaume wameamua Kutoa elimu kwa wanawake katika vijiji vyote vya kata ya yakobi wakianza na viongozi wa vijiji na kata pamoja na wanawake wanaoviwakilisha vikundi mbalimbali vya Kifedha.

"Lengo kubwa ni kujenga kwanza uelewa kwa viongozi na hawa wamama waweze kutambua haki zao zinazokandamizwa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi,na hivyo hivyo hata viongoziwaweze kutengeneza sera mbadala zitakazo weza kumkwamua huyu mwanamke aweze kuondokatana vitendo vya unyanyasaji vinavyotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi"   

Afisa maendeleo ya jamii kata  ya  yakobi bi.Renatha  nguli anasema ukatili ambao umekuwa Ukiripotiwa katika Ofisi za serikali ndani ya kata hiyo ni utelekezwaji wa familia na vipigo vinavyofanywa na wanaume licha ya wanawake wengi kuweka siri vitendo wanavyofanyiwa.

"Unakuta mtu amefikia hali mbaya ndio anakuja ofisini,hii ni kwa kuwa watu wengi wamekuwa wasiri,mpaka wanapigwa huko lakini kurepoti ni mara chache kuliko hizi za kutelekeza"alisema afisa maendeleo

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe ambaye ni diwani wa Kata ya yakobi Ester mgeni yeye pia anakiri kuwapo kwa ukatili kwa wanawake na watoto ndani ya kata yake jambo ambalo anatumia fursa hiyo kuwataka wanawake kupaza sauti pindi wanapofanyiwa ukatili.

"Lakini athari za kimazingira zipo ila bado huku kwetu ni wasiri hawawezi kusema kitu ambacho kinampata katika mazingira yake anayoishi lakini niwaombe tu wananchi kama watakuwa huru ni bora wakasema ili mambo mengine yaweze kusaidiwa"alisema bi.Mgeni

Aida ngewe ni mkazi wa Kijiji Cha Idunda  anasema sababu za wanawake kukaa kimya baada ya kufanyiwa ukatili ni kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza baada ya sauti wanazoweza kupaza huku   afisa mtendaji wa kijiji cha limage Bosco Mwenda  akisema kuwa ujio wa shirika hilo na kuwapa elimu wanaamini itakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili pamoja na kuwataka wanaume kuachana na Kuwanyanyasa wanawake.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post