China yaionya Marekani dhidi ya kutuma wanajeshi Mashariki ya Kati

China  imeionya Marekani baada ya kutangaza kutuma wanajeshi 1,000 wa ziada katika eneo la Mashariki ya Kati huku mvutano na Iran ukiwa unazidi kuongezeka. 

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa China Wang Yi pia ameisihi Iran kutojitenga na makubaliano ya nyuklia kiurahisi, baada ya nchi hiyo kusema itarutubisha madini ya Urani kwa kiwango kikubwa iwapo nchi zenye nguvu duniani zitashindwa kutimiza ahadi zake chini ya makubaliano hayo katika siku 10 zijazo.

 "Katika hali ya hivi sasa, tunatarajia kuwa Iran itafanya maamuzi ya busara na sio kuachana makubaliano kwa urahisi.  Wakati huo huo tunatarajia pande nyingine zitaheshimu haki na maslahi ya upande wa Iran na kuchukua hatua za kweli za kuilinda nchi hiyo." amesema Wang. 

Marekani iliongeza shinikizo lake dhidi ya Iran hapo jana, kwa kutangaza kutuma wanajeshi zaidi katika Mashariki ya Kati pamoja na kutoa picha kadhaa ambazo inasema ni ushahidi mwingine kwamba Iran inahusika na mashambulizi dhidi ya meli za kubebea mafuta yaliyotokea katika Ghuba ya Oman wiki iliyopita. Iran inakanusha vikali madai hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post