AJALI YAUA MMOJA NJOMBE, 22 WAJERUHIWA


Na Amiri kilagalila-Njombe
Gari la Abiria (Ibbu Trans) lenye namba za usajili T 225 DGF, Mitsubish Rosa linalofanya safari zake kutoka Njombe kuelekea wilayani Ludewa limepata ajali katika eneo la daraja la muholo wilayani Ludewa na kusababisha kifo cha mtu mmoja.


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe RPC Salumu Hamduni, amesema kuwa Ajali hiyo ilitokea Jana june 24/2019 majira ya saa Moja jioni, na Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Dereva aliyefahamika kwa jina moja la Chance ambae baada ya ajali alikimbia na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Amesema kuwa uchunguzi umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambae alishindwa kulimiliki gari na kuacha njia kisha kugonga gema na Kusababisha kifo cha mtoto mwenye umri wa miezi minne aliyefahamika kwa jina la Alvin Yohana Mtitu na Abiria 22 wamejeruhiwa.

Siku chache zilizopita Gari la Kampuni hiyo  linalofanya safari  kutoka kijiji cha Luvuyo wilayani Ludewa kuelekea Njombe mjini, lilipata Ajali na kupinduka maeneo ya Uwemba lakini halikusababisha madhara yeyote kwa abiria.

Mganga mkuu wa hospital ya wilaya ya Ludewa, Stanley Mlai amesema kuwa Hospital hiyo imepokea jumla ya majeruhi 22 Wanaume 7 na wanawake 15 ambao kati ya hao watano tayari wameruhusiwa, wawili wamepewa rufaa huku wengine wanaendelea na matibabu katika hospital hiyo.

Kufuatia tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Njombe ametoa wito kwa Madereva kuacha tabia ya kuendesha magari kwa spidi kali na kuwataka abiria na Jamii ya mkoa wa Njombe, kutoa ushirikiano pindi Madereva hao wanapokiuka sheria za usalama barabarani.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post