WALICHOKISEMA CHADEMA KUHUSU TUKIO LA MDUDE NYAGALI (MDUDE CHADEMA)


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika hali ya dharura, kinafuatilia kwa karibu, taarifa za Mdude Nyagali (Mdude Chadema) kuvamiwa kisha kuchukuliwa na watu ambao hawajatambulika, akiwa ofisini kwake, eneo la Vwawa, Mbozi, mkoani Songwe, katika tukio lenye dalili za utekaji.


Kwa mujibu wa baadhi ya mashuhuda, majira ya jana  jioni  (saa 12 kuelekea saa 1) yalifika magari mawili katika eneo la ofisini kwa Mdude, Vwawa mjini, kisha wakatelemka takriban watu wanne, ambao walimkamata kijana mmoja aliyekuwa nje ya ofisi hiyo wakampeleka kwenye mojawapo ya magari waliyokuja nayo huku wengine wakiingia ndani ya ofisi, alikokuwa Mdude.

Imedaiwa kuwa baada ya muda mfupi kulisikika purukushani, watu hao wakijaribu kumkamata Mdude huku wakimpiga na yeye akipiga kelele za kupinga kitendo hicho na kuomba msaada.

Taarifa za awali ambazo Chama kimezipata kutoka kwa mashuhuda hao zimedai kuwa baada ya kusikika kwa purukushani na kelele hizo, baadhi ya wananchi walijitokeza kutaka kujua kinachoendelea na kutoa msaada, ghafla watu hao waliokuwa wakimpiga Mdude wakatoa silaha aina ya bastola na kuwatishia wananchi hao, kitendo kilichowaogofya wananchi na kukimbia kwa hofu.

Imedaiwa kuwa watu hao walimuingiza Mdude kwenye ‘buti’ ya mojawapo ya gari hizo, wakamuachia yule kijana mwingine kisha wakaondoka na Mdude kuelekea kusikojulikana.

Tayari CHADEMA kupitia kwa Viongozi wa Chama katika eneo husika na Mbunge wa Mbozi Mashariki, Pascal Haonga, kimevitaarifu vyombo vya dola mkoani Mbeya, kwanza kutoa taarifa ya tukio hilo lenye mazingira ya utekaji pia kutaka kujua kama kuna askari waliopewa kazi ya kwenda kumkamata Mdude.

Hadi sasa haijulikani Mdude yuko wapi! Tupaze sauti zetu sote kulaani tukio hili na kutaka Mdude arudishwe au aachiliwe akiwa salama.

Katika hatua ya sasa, CHADEMA kwa nguvu zote kinalaani vikali tukio hilo. Tunavitaka vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi lenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, kufuatilia taarifa za tukio hilo kama zilivyoripotiwa kwa polisi katika eneo husika na kuhakikisha Mdude anapatikana na wahalifu waliotenda tukio hilo wanajulikana, kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Tutaendelea kuwapatia taarifa zaidi kadri itakavyohitajika.

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post