SERIKARI KUWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU UMOJA WA MATAIFA


Na Josephine Majura na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Katika kutekeleza ajenda za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s), Serikali imejipanga kuwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Hiari (VNR) katika Jukwaa la Siasa la Umoja wa Mataifa (HLPF) mwezi Julai mwaka huu mjini Newyork nchini Marekani.


Hayo yameelezwa na  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera), Bw. Adolf  Ndunguru wakati akifungua kikao cha kujadili Taarifa ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s).

Bw. Ndunguru alisema kuwa uwasilishwaji wa taarifa hiyo utakuwa ni wa kwanza miongoni mwa mfululizo wa taarifa za mapitio mengine ambayo yanatokana na mapitio hayo yanayoonesha namna nchi inavyotekeleza Malengo hayo.

Alisema kikao hicho ambacho kinahusisha wadau wa ndani na nje ya nchi, ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla kwa kuwa kitajadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) kwa kuangalia maeneo muhimu kama elimu, afya na uchumi.

Bw. Ndunguru alisema kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau hao kujadili rasimu ya awali ya taarifa ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) na kutoa nafasi kwa wadau hao kuchangia  maoni yao kuhusu namna ya kuboresha taarifa hiyo kabla ya kuiwasilisha Umoja wa Mataifa.

“Tukiwa kama wananchama wa Umoja wa Mataifa, tumekubali kuingia mkataba wa kuutekeleza  Maendeleo Endelevu katika ajenda ya 2030 , kwa lengo la kuboresha maisha ya watanzania, kwa kuhakikisha tunapeleka elimu bora, afya bora  na kuboresha miundombinu”, alisema Bw. Ndunguru.

Bw. Ndunguru alibanisha kuwa mpaka sasa Tanzania inatekeleza kwa kasi ajenda hiyo ya 2030 ya Maendeleo Endelevu  kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kutoa kipaumbele katika masuala ya elimu, afya na kukuza uchumi wa nchi.

Naye mdau wa mkutano huo ambaye ni  mwakilishi wa Umoja wa Asasi za Kiraia nchini, Prisca Kowa alilisema kwa sasa nchi inaonekana imejipanga kisawasawa kutekeleza Maendeleo Endelevu kwa kuwa imeweza kuyahusisha maendeleo hayo katika mipango mikubwa ya maendeleo ya nchi.

 Ametoa wito kwa Serikali, Wizara, Taasisi na wadau wa maendeleo  kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha taarifa sahihi za utekelezaji wa Maendeleo Endelevu zinapatikana kwa usahihi na kwa wakati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post