JINSI DUNIA YA INTANETI ILIVYOINGILIA MVUTANO KATI YA NDUGAI NA MASELE


Dunia ya sasa, ukisema kitu bila kueleweka vizuri, watu wa mitandaoni watatengeneza tafsiri yao. Utabaki unashangaa, mbona maana yako haikuwa inavyotafsiriwa na wengi?

Dunia ya intaneti, hasa unapokuwa kiongozi, unatakiwa ufafanue vizuri mawazo yako, vilevile utazame kipindi ambacho unajenga hoja, vinginevyo intaneti itakupeleka mahali ambako hukutaka.

Ndugai Vs Masele

Job Ndugai ni Spika wa Bunge la Tanzania. Stephen Masele ni mbunge wa Shinyanga Mjini. Masele pia ni mbunge wa Bunge la Afrika, vilevile Makamu wa kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika.

Sifa ya kuwa mbunge katika Bunge la Afrika ni lazima uwe mbunge katika nchi yako ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Ukiwa mbunge, ndiyo unaomba kuchaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Afrika. Ukipoteza ubunge kwenye nchi yako, moja kwa moja unakosa sifa za ubunge Bunge la Afrika.

Hapa ndipo kwenye mamlaka ya Ndugai. Kwamba Masele ni kiongozi wa juu kabisa Bunge la Afrika, lakini Ndugai anaweza kumfanya asiwe mbunge katika Bunge la Afrika kwa sababu ‘chaneli’ ya ubunge wake ni Bunge la Tanzania.

Ndani ya Bunge la Afrika kuna kashfa kumhusu Rais wa Bunge hilo, Roger Dang, raia wa Cameroon kutumia madaraka yake vibaya – kuhusika na rushwa ya upendeleo wa ajira na unyanyasaji wa kingono kwa watumishi.

Tuhuma dhidi ya Rais Dang (Spika) ni rasmi. Bunge la Afrika limezifanyia kazi na kamati ya uchunguzi imemtia hatiani Dang, ambaye alikuwa anajaribu kujinasua. Inadaiwa Dang baada ya kumuona Masele ni tatizo, alimshtaki kwa Ndugai.

Na Ndugai alimwita Masele nyumbani (Bunge la Tanzania) ajieleze. Awali, inadaiwa Masele alikaidi wito na akasema kwamba aliagizwa na Waziri mkuu, Kassim Majaliwa, apuuze wito wa Ndugai.

Kutokana na mvutano huo, Ndugai alitangaza kusimamisha kwa muda ubunge wa Masele kwenye Bunge la Afrika. Alimtuhumu kuwa anafanya mambo ya hovyo kugonganisha mihimili.

Baada ya kauli ya Ndugai na uamuzi wake, intaneti ilikuwa kinyume naye. Watoa maoni mitandaoni walimshambulia. Kwa mitazamo ya wengi, Masele yupo sahihi, maana tuhuma dhidi ya Dang ni nzito na anatakiwa kuwajibishwa.

Watu hawakuangalii kosa lililosemwa “kuchonganisha mihimili”, walijikita kwenye tuhuma za msingi zinazomkabili Dang.

Baada ya nivute nikuvute, Masele aliitikia wito. Kamati ya Maadili ya Bunge ilimkuta na hatia ya kugonganisha mihimili na kupendekeza aadhibiwe kwa kuzuiwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge. Hata hivyo Ndugai aliamua kumsamehe.

Pamoja na kutoa msamaha, mitandaoni Ndugai ameshahukumiwa kuwa anamtetea Dang, mwenye tuhuma. Akawa anamdhibiti Masele, anayepigania misingi.

Silioni kosa la Ndugai kumwita Masele alieleze Bunge la Tanzania kinachoendelea katika Bunge la Afrika. Nauona utovu wa nidhamu wa Masele kusema aliambiwa na Waziri mkuu akaidi wito wa Spika Ndugai. Matamshi hayo ni uchonganishi kwa Serikali na Bunge.

Pamoja na hivyo, Ndugai alipaswa kukumbuka yeye ni kiongozi katika ulimwengu wa intaneti. Angekumbuka hilo, angekuwa na angalizo kuhusu matamshi yake na uamuzi wake wa jumla kuhusu Masele.

Angejiuliza, je, tuhuma zipi ni nzito? Masele kukaidi wito au Dang kufanya unyanyasaji wa kingono na rushwa? Ukaidi wa Masele umeibukia wapi? Kabla, baada au katikati ya tuhuma za Dang? Majibu ni kuwa tuhuma za Dang ni nzito zaidi. Ukaidi wa Masele ulitokea katikati ya tuhuma za Dang.

Ndugai kwa kutambua yeye ni kiongozi katika ulimwengu wa intaneti, alipaswa kufahamu kwamba uamuzi wake kuhusu Masele ungesababisha sababu ya msingi izungumzwe. Na kwa sababu hiyo, alitakiwa kufahamu kwamba mitandao ingemhukumu kwa kumtetea Dang na kumdhibiti Masele.

Kuna swali; katika ulimwengu huu wa teknolojia ya habari na mawasiliano, ilishindikana vipi Ndugai kumpigia simu kuzungumza na Masele mpaka amwite nyumbani aache shughuli muhimu za Bunge la Afrika ikiwemo tuhuma za Dang?

Dunia ya intaneti yenye Skype, ilishindikana kufanya mkutano (Skype Meeting) kuondoa utata? Mwisho, Ndugai angeweza kulitatua suala la Masele kimyakimya, badala ya kupaza sauti. Kwa kuwa alizungumza, intaneti ikashtuka, ikatafuta sababu, ikaibuka na tafsiri kwamba Ndugai anamtetea Dang.

Busara za uongozi katika ulimwengu wa intaneti, zinataka ukumbuke kuwa kila unachofanya na unachosema, watu mitandaoni watapokea wanavyojua wao na watatafsiri kwa namna yao. Tafsiri yao itakuhukumu na itakukwaza. Hivyo, lazima uwe makini sana.
Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post