KISENA NA MKE WAKE WAKAMATWA TENA NA KUFUNGULIWA KESI YA UHUJUMU UCHUMI


Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena na mkewe,  Frorencia Mshauri Membe pamoja na wenzao watatu wameunganishwa katika kesi ya uhujumu uchumi wakikabiliwa na mashtaka 19 likiwamo la kuisababisha hasara ya Sh2.4bilioni kampuni ya Udart.


Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Chen Shi (32).

Watano hao  waliunganishwa pamoja katika kesi hiyo jana Jumatano Mei 15, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile na wakili wa Serikali, Grolia Mwenda.

Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni muda mfupi baada ya  washtakiwa hao waliokuwa wakikabiliwa na kesi mbili tofauti kufutiwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na Rwizile.

Uamuzi wa kuwafutia mashata ya awali ulitokana na upande wa  mashtaka kuomba chini ya kifungu cha 91 (1) cha mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA) sura 20 iliyofanyiwa marejeo 2002 kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)  hana nia ya kuendelea a kesi hizo, mahakama kuridhia.

Hata hivyo, waliendelea kushikiliwa na baadaye kusomewa kesi mpya ya uhujumu uchumi wakikabiliwa na mashtaka 19 ikiwa ni pamoja na kuongoza genge la uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali cha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), kuuza mafuta kwenye makazi yasiyoruhusiwa eneo la maegesho ya magari.

Mengine ni utakatishaji fedha, mashtaka manne ya kutoa nyaraka za uongo, mashtaka manne ya kughushi, mawili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kuahirishwa hadi Mei 28, 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post