WANNE WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUTUMIA JINA LA MAMA JANETH MAGUFULI KUTAPELI

Watuhumiwa wanne wa Dar es saalam wamefikishwa katika mahakama ya Kisutu wakituhumiwa kwa makosa manne ya matumizi mabaya ya mtandao ikiwemo kutapeli wananchi kupitia ukurasa wao wa Facebook kuwa wanatoa mikopo kupitia Taasisi waliyoitaja kuwa ni ya Mama Janeth Magufuli.


Pia washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha kiasi cha Sh4.5 milioni,Washtakiwa hao ni  Saada Uledi, Maftaha Shabani, Heshima Ally na Shamba Baila.

Akisoma hati ya mashtaka jana Alhamisi Aprili 18, wakili wa Serikali Batilda Mushi alidai washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 30/2019.

Alidai shtaka la kwanza ambalo ni kula njama, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2017 na Machi 2019 katika jiji la Dar Es Salaam walichapisha taarifa za uongo kupitia akaunti yao ya mtandao wa kijamiii wa Facebook.

Shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa siku na eneo hilo walichapisha machapisho katika akaunti yao ya mtandao wa kijamii wa Facebook, wakionyesha Janeth Magufuli ambaye ni mke wa Rais  Magufuli ameunda taasisi ya kutoa mikopo kwa watu mbalimbali ikiwa na masharti ya kuweka fedha kabla ya kupewa mkopo kama ni kinga ya mkopo huku wakijua kuwa ni uongo.

Shtaka la tatu, wanadaiwa Machi 2 na 8 mwaka huu jijini Dar es Salaam, wakiwa kama waendeshaji wa akaunti hiyo ya Facebook, walisajili akaunti hiyo kwa jina la Janeth Magufuli kwa nia ya kudanganya na kujipatia Sh4,487,000 kutoka kwa Paul Kunambi kama kinga  ya mkopo wakati wakijua kuwa siyo kweli.

Mushi ameendelea kudai katika shtaka nne ambalo ni utakatishaji wa fedha, washtakiwa kwa pamoja kati ya Machi 2 na 8 mwaka huu katika jiji hilo, walijipatia Sh 4, 487,000 huku wakijua kuwa fedha ni zao la  fedha haramu zilizotokana kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yanayowakabili, Hakimu Kasonde alisema hawatakiwi kusema chochote mahakamani hapo kutokana na kesi inayowakabili kuwa ni uhujumu uchumi.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 2 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527