UCSAF WAKABIDHI KOMPYUTA SIMIYU

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kompyuta 100 na vifaa vingine zikiwemo printa 10, vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 220.



Makabidhiano hayo yamefanyika Aprili 09, 2019 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na kushuhudiwa na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakuu wa shule na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi.

Akikabidhi kompyuta hizo Dkt. Yonaz amewapongeza viongozi mkoani Simiyu kwa kuendelea kufanya ubunifu katika masuala mbalimbali yanayouwezesha mkoa kukua katika nyanja mbalimbali hususani katika uchumi na elimu.

Aidha, amesema Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itaendelea kushirikiana na Mkoa wa Simiyu kuharakisha maendeleo kupitia Sayansi na Teknolojia.

" Ninaamini kompyuta hizi zitawasaidia sana wanafunzi hawa na walimu pia yapo mambo yatakayotatuliwa kupitia kompyuta hizi, ili tuweze kuleta elimu bora, tutengeneze wasomi wazuri ambao watachangia katika uchumi wa Taifa letu" , alisema Dkt. Yonaz.

Akipokea kompyuta hizo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameshukuru kwa msaada huo huku akibainisha kuwa lengo la Mkoa ni kuwa mkoa ambao uko kiganjani ambao taarifa yoyote inaweza kupatikana muda wowote.

“Tungehitaji mfahamu kuwa sisi ni miongoni mwa mikoa michache sana Tanzania yenye Mpango Mkakati wa TEHAMA wa mkoa na (focus) lengo letu kama mkoa ni kuwa mkoa ambao uko kiganjani, mkoa ambao mtu ataweza kupata taarifa yoyote wakati wowote”, alisema Mtaka.

Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF, Mhandisi. Peter Ulanga amesema UCSAF kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao inaandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa Maafisa TEHAMA ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kibunifu.

Nao walimu na wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Simiyu wameishukuru Serikali kutoa kompyuta hizo na kueleza namna zitakavyowasaidia.

"Kompyuta hizi kwanza zitatusaidia kuwezesha mawasiliano hususani katika masuala ya intaneti kwa ajili ya kutuma na kupokea taarifa mbalimbali kwa wakati na kuchapa majaribio ya wanafunzi" Mkuu wa Shule ya Sekondari Itilima, Mwl.Flora Shimbi.

"Vifaa hivi vitasaidia sana wanafunzi kujifunzia kwa vitendo wawapo shuleni na kutafuta 'notes' za masomo mbalimbali ili waweze kujifunza" Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Mwl.Ally Simba.

"Hizi kompyuta zitatusaidia kujifunza kwa vitendo na tutaelewa zaidi kuliko kama tungesoma bila kompyuta, kila atakachokuwa anafundisha mwalimu tutakuwa tunakiona moja kwa moja" alisema Naomi Mathias Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Bariadi.

Kompyuta hizo  pamoja na vifaa vingine vimekabidhiwa kwa baadhi ya Wakuu wa Taasisi, Ofisi za wakuu wa Wilaya, Ofisi ya mkuu wa mkoa na baadhi ya wakuu wa shule za Sekondari mkoani hapa mkoani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527