SIMBA YAENDELEZA UBABE...YAICHAPA KMC CCM KIRUMBA,YAISHUSHA AZAM FC

SIMBA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa 2-1 KMC, zote za Dar es Salaam katika mchezo uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 66 baada ya kucheza mechi 26 na kupanda hadi nafasi ya pili ikiizidi kwa wastani wa mabao tu, Azam FC inayoangukia nafasi ya tatu, huku Yanga SC ikiendelea kuongoza kwa pointi zake 74 za mechi 32.

Dalili mbaya kwa KMC zilianza kuonekana mapema tu, baada ya baada ya mchezaji wake, Aaron Lulambo kuumia dakika ya 20 na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Kelvin Kijiri.

Na dakika ya 22 mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi akaifungia Simba SC bao zuri akimalizia mpira wa adhabu wa kiungo Mghana, James Kotei kumtungua ‘Burundi One’, Jonathan Nahimana.

Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco aliikosa bao la awazi dakika ya 42, baada ya pasi ya kupewa pasi nzuri na mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere lakini akapiga shuti ambalo kipa Jonathan Nahimana alipangua na mpira ukagonga mwamba na kutoka nje.

Bocco tena akapewa pasi nzuri na Okwi dakika ya 45 na ushei, lakini akazidiwa mbio na beki wa KMC, Ismail Gambo ‘Kussi’ aliyefanikiwa kuutoa mpira nje na kuwa kona.

Kipindi cha pili, KMC walikianza vizuri na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha, mfungaji Hassan Salum Kabunda dakika ya 57 aliyemchambua vizuri ‘Tanzania One’, Aishi Manula baada ya kumtoka beki Mburkinabe, Zana Coulibaly kufuatia pasi ya George Sangija.

Simba SC wakapoteza nafasi ya kupata bao la ushindi dakika ya 62 baada ya mshambuliaji wake, Mnyarwanda Kagere kukosa penalti kufuatia shuti lake kudakwa na kipa, Jonathan Nahimana aliyeiwezesha Burundi kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza mwaka huu nchini Misri.

Penalti hiyo ilitolewa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga baada ya kiungo wa KMC, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ kuunawa mpira uliopigwa na Okwi kwenye boksi.

Dakika ya 69 Simba wakawa wenye bahati baada ya refa Kambuzi kuwanyima penalty KMC kufuatia Emmanuel Okwi kuunawa mpira uliopigwa na Kabunda kwenye boksi na kuwaacha mashabiki wakiimba ‘Refa Refa Refa’. 

Nahodha Bocco akawazidi mbio mabeki wa KMC kwenye boksi dakika ya 74, lakini akiwa anatazama na kipa Nahimana akapiga nje na kukosa bao la wazi, ingawa ajabu refa akawapa kona Simba.
Kambuzi akawapa tena Simba SC penalti dakika ya 82 baada ya Cabaye kugongwa tena na mpira mkononi na Bocco akaenda kuifungia Simba SC bao la ushindi na kuwaamsha mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi waliokuwa wameanza kukata tamaa.

Kikosi cha KMC kilikuwa; Jonathan Nahimana, Aaron Lulambo/Kelvin Kijiri dk20, Ally Ramadhani, Ismail Gambo, Yusuph Ndikumana, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, George Sangija/James Msuva dk58, Abdul Hillary, Omary Issa, Hassan Kabunda na Ally Msengi. 

Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Etasto Nyoni, James Kotei/Muzamil Yassin dk63, Clatous Chama/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk86, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi/Hassan Dilunga dk77.
Chanzo - Binzubeiry 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527