SERIKALI MBIONI KUANZA MPANGO WA UAGIZAJI WA GESI YA MITUNGI (LPG) KWA PAMOJA


Serikali imesema iko katika hatua za awali za kuandaa mpango  wa uagizaji wa gesi ya mitungi (LPG) kwa pamoja kama ilivyo kwa mafuta ya Petroli hali itakayosaidia kudhibiti masuala mbalimbali ikiwemo  bei ya gesi hiyo.

Akizungumza wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, wananchi katika maeneo yote nchini wanafikiwa na huduma hiyo, hivyo Serikali itaratibu usambazaji wa gesi hiyo badala ya kuwaachia wauzaji wenyewe kuamua maeneo  wanayotaka kupeleka gesi.

‘’ Serikali ikitangaza bei elekezi kulingana na soko, itawafanya wauzaji wafuate bei hiyo badala ya wao kujipangia, hii itasaidia wananchi kuuziwa gesi kwa gharama inayofanana katika maeneo mbalimbali ambapo gesi hiyo itauzwa.”alisema Dkt. Kalemani.

Alieleza kuwa, suala la sasa la kila muuzaji kujiamulia sehemu anayotaka kupeleka gesi inafanya maeneo mengine kukosa kabisa nishati hiyo hivyo sasa Serikali itaweza kuwadhibiti wauzaji na kuhakikisha kuwa maeneo yote nchini yanafikishiwa gesi.

Aliongeza kuwa, utaratibu wa kuagiza gesi inayotumika  majumbani kwa pamoja utasaidia Taifa kutambua kiwango halisi cha gesi kinachohitajika nchini na kiasi cha gesi kinachoingizwa nchini na hivyo kusaidia pia katika shughuli za ukusanyaji wa mapato.

Awali, akitoa taarifa kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja  (PBPA), Erasto Simon  alisema kuwa, Wakala huo kwa sasa unafanya tathmini ya namna bora ya kuanza uagizaji wa pamoja wa gesi ya mitungi (LPG) kwa kuzingatia maoni kutoka kwa  wadau mbalimbali.

Akizungumzia faida mbalimbali zinazotokana na uagizaji wa mafuta wa pamoja, Simon alisema kuwa, ni kuweka mazingira sawa ya kibiashara kwani gharama za uagizaji wa mafuta ziko sawa kwa makampuni yote na kuondoa mianya ya rushwa katika uagizaji wa mafuta kwani ufunguzi wa zabuni hufanyika kwa uwazi na washiriki wote huridhika na matokeo ya zabuni.

Alitaja faida nyingine kuwa ni, Taifa kuwa na uhakika wa usalama wa upatikanaji wa mafuta kwa muda wote na kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za mafuta zinazosaidia katika ukusanyaji wa mapato na kupanga bei elekezi ya mafuta.

Aliongeza kuwa, mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umewezesha nchi kudhibiti ubora wa mafuta yanayoingia nchini na pia kuongezeka kwa sehemu za kupokelea mafuta kama  bandari ya Tanga na Mtwara, tofauti na ilivyokuwa awali kwani Bandari ya Dar es Salaam ndiyo ilikuwa ikitumika kwa shughuli hizo.

Kutokana na hilo, alisema kuwa, nchi mbalimbali barani Afrika kama vile Malawi, Zambia na Msumbiji wamekuja kujifunza kuhusu mfumo huo wa uagizaji  mafuta ili waweze kuutumia katika nchi zao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post