RAIS MAGUFULI ABADILI MATUMIZI YA ENEO LA UWANJA WA NDEGE MBEYA NA KULIFANYA KUWA LA WAMACHINGA


 Rais John Magufuli amebadili matumizi ya eneo la uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya na kulifanya kuwa la wamachinga kufanyia shughuli zao.

Amesema amechukua uamuzi huo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao ndogo kufanya biashara zao katikati ya mji, huku akiagiza mikoa yote kutenga maeneo kwa ajili yao.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana mjini Mbeya wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano inayoendelea mkoani humo.

Alisema kuanzia sasa eneo hilo litengenezewe miundombinu ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao katika mazingira mazuri ikiwemo vyoo, kituo cha mabasi na litakalobaki lijengwe kituo cha uuzaji madini.

Rais alitoa agizo hilo baada ya kupokea maombi ya viongozi wa mkoa huo wakitaka kutengwa eneo maalumu kwa wamachinga ambao wanafikia 350,000 ili wafanye biashara zao kwa utaratibu mzuri tofauti na sasa wanavyojipanga kila mahali.

“Hili eneo nimelitoa bure, nendeni mkafanye biashara, lakini haina maana yale maeneo mengine mliyokuwa mnakaa msiende, endeleeni na shughuli zenu kote, wamachinga ndio walionipa kura na niliahidi kuwatetea, nitawatetea wafanye biashara zao,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527