MTWARA HALI SI SHWARI KIMBUNGA KENETH



Wakazi wa baadhi ya maeneo mkoani Mtwara wameendelea kuyahama makazi yao, baada ya kuwepo kwa tahadhari ya kuwepo kwa kimbunga kikubwa cha Keneth katika maeneo hayo.

Taarifa kutoka mkoani Mtwara zinasema kwamba wakazi hao wamekuwa wakitumia vyombo mbali mbali vya usafiri na wengine kulazimika kutembea kwa miguu, kukimbilia maeneo yaliyotangazwa na serikali yenye miinuko ya Naliendele, maeneo ya Uwanja wa ndege Mtwara na kambi za jeshi za JWTZ Naliendele, ambako kumetajwa kuwa ni salama.
Hali ilivyo sasa Mtwara

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mikindani, Evodi Mmanda, amesema kwamba dalili za kimbunga hicho zimeshaanza kujionesha kwa kuwepo kwa mvua, na kutanda kwa wingu kubwa.

 “Dalili zilizozungumzwa zimeshaanza kujionesha, wingu limefunga, imeanza mvua kidogo kidogo tangu asubuhi, na tumeambiwa huo ndio mwanzo wake unavyokwenda.

......, na tumeambiwa kimbunga kinakwenda kwa kasi, km 70 kwa saa, kinaenda mpaka 120 mpaka 150, ni kasi kubwa sana ambayo hata gari huwezi kulikimbiza kwa kasi hiyo, na kimeandamana na mvua, radi, kunaweza kukatokea madhara. Tunaposema watu waende kwenye maeneo yenye miinuko ni kwamba waweze kuokoa maisha yao pindi janga hili litakapotokea, lakini tunaombea lisitokee”, amesema Mheshimiwa Mmanda.

Hata hivyo taariza zaidi zinasema kwamba maeneo ya mpakani mwa Msumbiji na Tanzania tayari mvua kubwa inanyesha ambayo inahofiwa huenda italeta mafuriko.

Hapo jana Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa taarifa ya kuwepo kwa kimbunga kikubwa kitakachotokea katika maeneo ya Pwani ya mikoa ya Lindi na Mtwara, na kuwataka watu kuchukua tahadhari na kuhama maeneo ya ufukweni, huku Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kuagiza wafanyakazi wasiende kazini na wanafunzi wabaki nyumbani, ili kuangalia usalama wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527