CCM MKOA NJOMBE YAWAOMBA WANACHI KUJITOKEZA KUMPOKEA RAIS MAGUFULI


Na Amiri Kilagalila-Njombe
Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kimetoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli  katika maeneo mbali mbali ikiwemo barabarani pamoja na maeneo ya mikutano mara baada ya kiongozi huyo atakapowasili  kwa ziara yake ya kikazi.

Wito huo umetolewa na katibu mwenezi wa chama hicho mkoa Ndugu Erasto Ngole,wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya ujio huo wa kiongozi wa kitaifa kwa mara ya kwanza mkoani Njombe na baadhi ya mikoa ya nyanda za juu kusini tangu alipochaguliwa.

Aidha Ngole amewataka wanachama wa chama cha mapinduzi kujitokeza katika mapokezi hayo wakiwa na sare za chama kwa kuwa kiongozi huyo pia ni mwenyekiti wa chama ngazi ya Taifa.

“Tukumbuke kwamba mheshimiwa anayekuja ni mwenyekiti wa chama cha mapinduzi taifa ni Rais ambaye anatekeleza ilani ya chama cha mapinduzi,sisi wana CCM ndio wenye mtu wetu namba moja tuliomtuma tuliompa tiketi yetu, naomba Tujitokeze kwa wingi tukiwa kwenye uniform ya chama cha mapinduzi”alisema Ngole

Kwa upande wake katibu wa hamasa na chipukizi mkoa wa Njombe UVCCM ndugu Elly Johnson Mgimba,amesema kutokana na shughuli kubwa ya kujenga uchumi wa Taifa iliyofanywa na kiongozi huyo, anatoa hamasa kwa vijana wakiwemo boda boda na mama ntilie kufika kumlaki Magufuli kwa kuwa amewatetea kwa kiasi kikubwa.

“Wengi tunajua ni ziara yake ya kwanza toka aingie madarakani lakini matunda ya serikali tumeyaonja na tunayaishi ikiwemo kushughulika na wabadhilifu,elimu bure na mambo mengine Mengi,kikubwa niwahamasishe vijana wenzangu boda boda mama ntilie ambao kwa kiasi kikubwa ameyagusa maisha yetu,sasa tuna kila sababu ya kumlipa kwa kuonyesha uzalendo wetu”alisema Johson Mgimba

Baadhi ya wananchi mkoani Njombe akiwemo mzee Lukure wameshukuru ujio wa kiongozi huyo kwa kuwa ni mara ya kwanza kufika mkoani humo huku wakimuomba Rais kuwa na neno juu ya miradi ambayo haijaenda vizuri.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John pombe Magufuli,anatarajia kufanya ziara ya siku Tatu mkoani Njombe baada ya kutokea mkoani Ruvuma na kukagua baadhi ya miradi mikubwa ikiwemo ya barabara na hospital.

Akizungumza jana na vyombo vya habari  alisema Rais Magufuli atafanya ziara ya siku Tatu kuanzia tarehe 09-11/04/2019.

Olesendeka alisema kuwa katika Ziara hiyo atatembelea na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo na kuongea na wananchi.

“Mheshimiwa Rais siku ya kwanza atapokelewa na viongozi wa serikali, chama pamoja na wananchi katika mpaka wa mkoa wa Njombe na mkoa wa Ruvuma  siku ya tarehe 9 mchana na kwenda katika eneo la uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata chai cha kabambe Tea factory inayomilikiwa na kampuni ya Uniliver  Plc ya London nchini Uingereza  kwa pamoja na kampuni ya Uniliver  nv ya Roturdam nchini Netheland, na kufanya kazi mbili kubwa ikiwemo kuzindua kiwanda hicho na kuzungumza na wananchi watakao kuwepo katika eneo la kiwanda hicho,na baada ya hapo ataondoka kupitia barabara ya Njombe-Songea kwenda katika eneo lake la kupumzika la ikulu ndogo ya Njombe”alisema Olesendeka

Siku ya pili Rais atafanya kazi mbili kubwa ambazo ni kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospital ya Rufaa ya mkoa wa Njombe katika eneo la kutolea huduma za nje (OPD)   uliokamilika kwa asilimia 95 na imegharimu kiasi cha Tshs.Bilioni 3.6

Aidha ataweka jiwe la Msingi katika barabara inayounganisha makao makuu ya mkoa wa Njombe na wilaya ya Makete yaani Njombe -Moronga-Makete  katika eneo la shule ya msingi ya Ramadhani inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya takribani Tshs.Bilioni 217 ikiwa ni moja kati ya miradi ya barabara za lami na zege zinazojengwa mkoani Njombe yenye thamani ya zaidi ya Tshs.Bilioni 480 pamoja na kufanya mazungumzo na wananchi katika viwanja vya shule ya msingi Ramadhani.

Katika hatua nyingine Olesendeka amesema kuwa,

 “Siku ya Tatu ya ziara ya Rais Magufuli ambayo ni tarehe 11 ya mwezi wanne atapata fursa ya kufungua mradi wa ujenzi wa barabara ya Mafinga-Nyigo -Makambako-Igawa eneo la mpaka wa Makambako na wilaya ya Wanging’ombe ambao ni kilometa 64.6 uliojengwa kwa kiwango cha lami ya kisasa na kugharimu Tshs.Bilioni 103,432,947,407.64 na baadaye katika eneo hilo la makambako atapata fursa ya kuzungumza na wananchi wa miwili watakao kuwa wamehudhuria katika uzinduzi wa mradi huo wa barabara”alisema Olesendeka


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527