WANAWAKE WASEMA MAFANIKIO CHANYA YANAHITAJI USHIRIKISHWAJI WA WANAWAKE

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsi (TGNP) Lilian Liundi 

Wanawake kutoka taasisi mbalimbali wamesema kuwa mafanikio ya kiuchumi, kifikra, kielimu na afya yanahitaji ushirikishwaji wa mwanamke ili yawe chanya.

Wakizungumza leo Ijumaa Machi mosi kwenye mkutano wa siku moja wa kujadili mafanikio yaliyopatikana baada ya miaka 25 ya mkutano wa Beijing.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsi (TGNP) Lilian Liundi amesema kuwa licha ya fursa nyingi kwa wanawake kufunguka bado ushirikishwaji kwenye baadhi ya mambo unahitaji msukumo.

"Changamoto zimepungua lakini unyanyasaji wa kijinsia, fursa za kumiliki mali, fursa za kukua kiuchumi bado zinahitaji msukumo wa wanawake," amesema.

Amefafanua ili kufikia mafanikio ikiwamo malengo ya Milenia ipo haja ya kuendelea kuwainua wanawake kielimu, kiuchumi na kuwapa nafasi ya kutoa maoni na mawazo yao kwenye maamuzi ya mambo yanayohusu nchi yao.

"Nafasi hizo zipo chache na zinawafikia wachache hususani waliopo mijini, hivyo ili kujenga uelewa kwa wanawake wote nchini ipo haja ya nafasi hizo za kutoa maoni, mawazo ushauri na kushiriki kwenye maamuzi zifike kila kona ya nchi," amesema Liundi.

Amesema kupitia mkutano huo watajadili misingi ya mkutano wa Beijing, ambapo muhimu lilikuwa ni kuweka usawa, kuondoa dhana potofu juu ya haki za mwanamke.

Kwa upande wa mwanzilishi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Marry Lusimbi amesema kuwa mkutano wa Beijing ni wa kukumbukwa kwa sababu umefungua fursa ya wanawake kudai haki zao popote walipo na kilichobaki ni kuhakikisha Serikali inakwenda nao pamoja ili kupata matokeo chanya katika mipango ya maendeleo.

Amesema kabla ya mkutano huo hakukuwa na nafasi ya mwanamke kujitokeza hadharani na kutetea jambo lolote linalohusu haki zake.

"Aliyefanya hivyo alionekana amekiuka dini, jamii, na asiyestahili kuolewa, lakini sasa harakati za kumkomboa mwanamke zinatambulika duniani kote," amesema na kuongeza.

"Wakati tunarudi Beijing Rais alikuwa Benjamini Mkapa, alipokea ripoti tuliyorudi nayo na mambo yaliyokuwemo yanafanyiwa kazi kisera, kibajeti , lakini kuna wenzetu ikiwamo Kenya wakati huo Rais alikuwa Moi aliwaambia Beijing yao waiache huko huko uwanja wa ndege, hivyo ilikuwa bahati kwetu na mafanikio yanaonekana kwenye baadhi ya maeneo, wanawake wanaweza kupaza sauti na wakasikilizwa," amesema Lusimbi.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo waliyajadili na sasa yamefanyiwa kazi hadi kwenye bajeti ni pamoja na suala la usawa maarufu 50 kwa 50.

Kwa upande wa Mary Ndaro kutoka Care International amesema kuwa wanawake ndiyo wazalishaji wakuu hivyo wasiposhirikishwa mpango wa 20/25 utabaki ni mpango tu na hautatekelezeka.

Amesema mwanamke akishirikishwa kwenye jambo hususani la kitaifa uelewa na utekekezaji kwenye jamii unakuwa mkubwa na wenye ufanisi kwa sababu wapo kwenye nyanja zote ikiwamo kuijenga jamii.

Na Kalunde Jamal, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post