MKUU WA MKOA WA PWANI AZIKARIBISHA KAMPUNI 13 ZINAZOTAKA KUJENGA VIWANDA


Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza mbele ya Waandishi wa habari mwishoni mwa wiki ,mara baada ya kumaliza kikao cha pamoja wakati wa majadiliano
kati ya wawekezaji kutoka China, viongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na idara nyingine serikalini zinazohusika na  uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geofrey Mwambe akisalimiana na mmoja wa wekezaji mara  baada ya kumaliza kikao chao cha pamoja na Mkuu wa Mkoa  Mhandisi Evarist Ndikilo. 
Mwakilishi wa kundi la wawekezaji hao ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni  ya Sinoma East Africa Co. Limited, Lu Xiaoqiang akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu kwanini wameichagua  Tanzania kuwekeza,ambapo alieleza kuwa wanaamini kuna fursa nyingi za uwekezaji na kwa muda 
wa miaka 10 waliyofanya kazi nchini wamevutiwa na namna watanzania  walivyo wakarimu.
Mkurugenzi wa Makampuni ya Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa habari mwisho mwa wiki Kibaha mkoani Pwani,mara baada ya kumaliza kikao chao cha pamoja.
Baadhi ya wadau wa maendeleo ya uwekezaji wa Viwanda mkoa wa pwani,kwamati ya Ulinzi na usalama wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa  Mhandisi Evarist Ndikilo,wakati wa majadiliano
kati ya wawekezaji kutoka China, viongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na idara nyingine serikalini zinazohusika na  uwekezaji.
Picha ya pamoja
***

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

SERIKALI ya Mkoa wa Pwani,kupitia Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo amesema hawako tayari kuzikosa kampuni 13 ambazo zimepelekwa mkoani kwake kutokana na jitihada za Mkurugenzi wa Makampuni ya Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa.

Mhandisi Ndikilo amebainisha hayo ofisini kwake baada ya majadiliano kati ya wawekezaji kutoka China, viongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na idara nyingine serikalini zinazohusika na uwekezaji.

Ambapo Mhandisi Ndikilo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia juhudi ambazo zinafanywa na Kiluwa za kuleta wawekezaji kuwekeza mkoani humo zikiwemo Kampuni hizo 13 ambazo zimekuja kuwekeza na wamepata baraka za mkoa wake.

Amefafanua baada ya kikao cha majadiliano Mhandisi Ndikilo amesema kazi iliyobaki ni kuangalia namna wawekezaji hao watakavyomalizana na mamlaka nyingine za nchi ili kufuata taratibu zinazotakiwa.

"Hawa watu wamejipanga kuwekeza katika viwanda mbalimbali 13, mtaji wanao wapo tayari kuanza hata kesho. Naagiza kila idara ifanye kazi yake ili hawa wawekezaji tusiwakose," amesema Mhandisi Ndikilo.

Katika maelezo yake kutokana na kutumia muda wa zaidi ya saa sita kujadiliana kuhusu mustakabali wa wawekezaji hao wakiwa na kamati ya ulinzi na usalama na maofisa mbalimbali wakiwemo wa TIC na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Ndikilo alisema:

“Fursa na sifa tulizonazo kama mkoa kunavutia wawekezaji wengi, ila kama tunavyofahamu uwekezaji haufanyiki angani bali kwa kutumia ardhi, kulikuwa na mvutano kuhusu ardhi ndio mana tumetumia muda mwingi kujadiliana.

“Vilevile tumejadili mambo mengi kuhusu aina ya uwekezaji mkubwa unaotaka kufanyika, sote tumeridhia namna walivyojipanga wamekuja na mitaji mikononi na aina ya bidhaa na huduma watakazozalisha, wanataaka kuhamisha teknolojia kutoka China kuja Tanzania. Ndiyo maana nimetoa wiki mbili majibu yapatikane hawa wawekezaji waanze kazi.”

Akizungumzia eneo la uwekezaji la Kiluwa Free Processing Zone, Mhandisi Ndikilo amesema hatakubali kuona wazo hilo la mtanzania mzalendo linapotelea hewani wala kuona wawekezaji wanakwenda nchi jirani kwa kukimbia mizengwe nchini.

“Mkoa wetu una ardhi kubwa ya uwekezaji, Kibaha ina maeneo mengi nay a kutosha hata kule Mlandizi tuna ekari zaidi ya 5,000 hazijaguswa. Hivyo, nataka waelewe Mkoa wetu ni wa amani ndio mana tumeiita na kamati ya ulinzi na usalama ishiriki mkutano huu.

“Serikali inataka kuipeleka nchi katika uchumi wa kati kwa kutegemea viwanda, sasa tukiona watu wenye nia ya kuanzisha viwanda wanasumbuliwa hatuwezi kukaa kimya. Taratibu zote wamefuata lakini ikionekana mkoa wangu ndio kikwazo sitakubali,” amesema Mhandisi Ndikilo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geofrey Mwambi alisema kazi ya kuleta wawekezaji ni ya serikali. Hivyo, wanavyoona watu wanaisaidia serikali hawawezi kuwavunja moyo.

"Hawa ni wa mwanzo tu wapo wengi, kati ya hao 13 tayar wawekezaji sita wameshakuja na vifaa vyao wanasubiri kupewa ruhusa waanze kazi. Kuna viwanda vya Battery, bidhaa za ngozi na mabehewa," anasema Mwambi.

Mwakilishi wa kundi la wawekezaji hao ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sinoma East Africa Co. Limited, Lu Xiaoqiang alisema wameichagua Tanzania kwa kuwa wanaamini kuna fursa nyingi za uwekezaji na kwa muda wa miaka 10 waliyofanya kazi nchini wamevutiwa na namna watanzania walivyo wakarimu.

“Tupo tayari kushirikiana na watanzania na kuwafundisha ujuzi wa mambo mbalimbali, tunataka kuanzisha viwanda vya bidhaa za plastiki, chuma, battery na vifaa vingine vya kielektroniki. Tunahamisha utaalamu kutoka China kuja Tanzania,” alisema Xiaoqiang.

Naye Kiluwa amesema TIC inawaelekeza nini cha kufanya hivyo hawawezi kuwaangusha na wataendelea kufanya kazi nao kadiri ya uwezo wao.“TIC kazi yao imeshakamilika, huwa wanatupatia elimu ili kufuata taratibu zinazostahiki kusajili wawekezaji, naishukuru serikali ya Mkoa wa Pwani kwa msaada mkubwa iliyotoa kwetu na kukubali kutusikiliza hadi kuelewa lengo letu katika uwekezaji.

“Kuna zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 100 zinataka kuwekezwa hapa, hiyo ni fursa ya ajira na Mamlaka ya Mapato Tanzania itaongeza mapato. "Hawaii wawekezaji wamejipanga hawana muda wa kupoteza, kati ya viwanda 13 wawekezaji sita tayari wameshaleta hadi vifaa wanasubiri kupewa ruhusa tuwaanze kazi,” alisema Kiluwa.

Amesema ni jukumu la Watanzania kila mmoja kwa nafasi take kuhakikisha maono ya Rais Dk.John Magufuli ya kuhamasisha ujenzi wa viwanda unafanikiwa kwa vitendo,hivyo mkakati wake ni kuendelea kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

"Nina ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji,hivyo wawekezaji ninapowamasisha kuja nchini kuwekeza pia nawaeleza na uwepo wa ardhi na wakija nchini wanakwenda TIC ambako ndiko watapewa utaratibu kwani niliamua hati ya ardhi niliyonayo kwa ajili ya uwekezaji iwe wazi kwa TIC pia," ameongeza.

Amesisitiza katika kufanikisha uwekezaji kwake anaona ni jambo jema kwani kikubwa anachoamini mbali ya watanzania kupata ajira,teknolojia ambayo inaletwa na wawekezaji itabaki nchini kwa maslahi ya Watanzania.",Ninachokifanya ni kama nang'oa teknolojia nje naileta nyumbani."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527