HAKIMU AAHIRISHA KESI KISA HARUFU YA POMBE SINGIDA


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Stela Kiama, ameahirisha kesi baada ya mmoja wa washtakiwa kwenye kesi ya wizi, kuingia mahakamani akiwa amelewa chakari. 


Kesi hiyo ya wizi na kuharibu mali inayowakabili wakazi watatu wa tarafa ya Itigi, wilayani Manyoni, ilikuwa isikilizwe jana lakini ilishindikana kutokana na kisa hicho.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni Mussa Haruna (47), Yohana Simon (42) wote wakazi wa Mtimkavu na Joseph Alphonce (39) mkazi wa Mlowa.

Majira ya saa 7:30 mchana, Karani wa Mahakama aliwaita washtakiwa hao ili waingie ndani ya mahakama hiyo kwa ajili ya utetezi wao lakini walipoingia Hakimu alimshtukia mshtakiwa mmoja kwamba amelewa na hajiwezi.

Baada ya washtakiwa hao kuingia mahakamani hapo, Hakimu alihisi harufu kali ya pombe mahakamani na mahojiano kati ya Hakimu na mshtakiwa huyo yalikuwa kama ifuatavyo;- 

Hakimu: Mshitakiwa namba mbili vipi mbona unapepesuka na unaonekana hauko sawa. Unaonekana kabisa umelewa pombe, hivi kweli utaweza kusikiliza kesi yako?

Mshitakiwa: Mheshimiwa Hakimu mbona mimi niko vizuri tu na wala si kama nimekunywa pombe leo (jana) asubuhi. Hizi ni za jana na nina uwezo wa kusikiliza kesi yangu bila tatizo lolote lile.

Hakimu: Hivi Mwendesha Mashtaka kama mimi tu niliyekaa mbali na mshtakiwa nasikia harufu kali kiasi hiki je, wewe ambaye uko karibu naye itakuwaje?

Mwendesha Mashata: Hata mimi Mheshimiwa Hakimu nasikia kabisa harufu ya kilevi alichokunywa mshitakiwa huyu na kwa kweli namwona hayuko ‘serious’ (makini) na kesi inayomkabili.

Hakimu: Hivi wewe mshitakiwa una uwezo wa kuendelea kusikiliza kesi yako au tuahirishe shauri lako mpaka siku nyingine utakapokuja ukiwa hujanywa mipombe yako?

Mshitakiwa: Mheshimiwa Hakimu nakuthibitishia kwamba nina uwezo kabisa wa kuendelea na shauri langu kwa sababu hizi pombe sijanywa leo (jana) asubuhi wakati nakuja mahakamani. Nilikunywa jana ingawa leo bado naonekana kama bado zipo kichwani.

Hakimu: Wewe mshtakiwa usipende kuwaudhi watu kwa mambo yako ya ajabu. Hivi unadhani sisi sote hatuna uwezo wa kufahamu mtu aliyekunywa kilevi na ambaye hajanywa kilevi?

Mshitakiwa: Si mheshimiwa Hakimu, mimi nakuruhusu uendelee kusikiliza shauri hili na mimi nitajitetea kwa kadiri ya uwezo wangu.

Hakimu: Mshitakiwa nakupa onyo mara ya mwisho na iwapo utarudia tena kutenda kosa kama hili nitakufutia dhamana yako ili upelekwe mahabusu ukajifunze zaidi kutii sheria za nchi. 

Utakapokaa gerezani ndipo akili yako itakuwa sawa maana hautapata muda wa kunywa mataputapu yako kama unavyofanya sasa na utakapokuja mahakamani utakuwa na uwezo wa kujitetea kama wengine. Usitake kutuchefua watu wengine huwa hatutaki kuongea sana na usidhani wewe ndiye una akili kupita watu wengine hapa mahakamani. Mimi naweza kukubadilikia muda si mrefu halafu usije kunilaumu.

Baada ya mshitakiwa huyo kupewa onyo, Hakimu aliwauliza washtakiwa wengine kama watakuwa tayari kuendelea na kesi na walikubali.

Ingawa washtakiwa hao walimruhusu kuendelea, Hakimu aliposhauriana na mwendesha mashtaka, walikubaliana kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 12, mwaka huu.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Septemba 17, 2017 majira ya saa 3:00 asubuhi katika Kijiji cha Kitopeni, washitakiwa waliiba alama tano za barabarani zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 4.8.

Kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka 2017 imefikia hatua ya washtakiwa kuwasilisha utetezi wao mbele ya mahakama pamoja na kupeleka mashahidi.
CHANZO - NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post