LOWASSA : NIMETAFAKARI NA KUAMUA KURUDI NYUMBANI... "CCM WACHEKELEA KILA KONA


Mwenyekiti wa CCM,Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu wa zamani Mh.Edward Lowassa mara baada ya kutangaza kurejea CCM leo kwenye ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijin Dar es salaaam.


WAZIRI Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Edward Lowassa ametangaza rasmi kurudi Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuanzia leo Machi 1,2019.

Lowassa aliondoka CCM na kwenda upinzani katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) wakati wa mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.Aliondoka CCM na kwenda upinzani baada ya jina lake kukatwa katika kugombea urais kupitia Chama hicho.

Hivyo alipata ridhaa ya kugombea nafasi ya Urais kupitia Chadema waliokuwa wameunganisha nguvu na vyama vingine vinne vya siasa vilivyokuwa vimeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Akiwa upinzani Lowassa aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema lakini kuna kipindi aliamua kwenda Ikulu kufanya mazungumzo na Rais Dk.Magufuli ambapo baada ya kukutana na Rais alisema amevutiwa na utendaji kazi wake na anampongeza.

Akizungumza leo katika Ofisi za ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam,Lowassa hakuwa na maneno mengi ya kueleza zaidi ya kuwaambia Watanzania kuwa ameamua kurudi nyumbani (CCM).

"Nimetafakari na sasa nimeamua kurudi nyumbani CCM ambako sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa huko,"amesema Lowassa huku mamia ya wananchi wakiwamo wanachama na wapenzi wa CCM walikuwa wanamshangilia.

Wakati Lowassa anatangaza kurejea CCM alikuwa amesikindikizwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga ambaye pia aliwahi kuwa Mtunza wa fedha wa CCM Rostam Aziz.

Akizungumza baada ya Lowassa kurudi CCM, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli amesema wamempokea Lowassa na katika kuthibitisha hilo waliona ni vema uamuzi wake akautangazia Ofisi za CCM Lumumba kama sehemu ya uthibitisho.

"Kama ambavyo amezungumza kwa kifupi mwenye Mzee Lowassa kwamba amerudi nyumbani ambako ni huku CCM, tumempokea.Amekuja kutangazia hapa Lumumba kama sehemu ya kutoa shuhuda.

"Kwa upande wetu tumekaa, tumefakari na kujiridhisha Lowassa amekaa kwenye Chama kwa muda mrefu na kwa bahati mbaya zilizojitokeza aliamua kwenda upinzani.Tumemsikiliza mawazo yake kwamba amekaaa kwenye Chama Cha Mapinduzi sehemu kubwa ya maisha yake na kwamba kutokana na sababu ambazo amezieleza aliamua kwenda upinzani na leo hii amerudi nyumbani,"amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo kabla ya Rais Magufuli kuzungumza aliamua kuwatania watu waliokuwa wamejitokeza Lumumba na kuwaambia imekuaje wako hapo au wanamaono na hivyo walijua kitakachotokea.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally amesema Lowassa amefikia uamuzi wa busara kwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kushirikiana katika kuleta maendeleo ya wananchi wote.

"Amerudi nyumbani, kwa hiyo tunaanza kazi ya kujenga Taifa letu na kujenga utu wetu, Lowassa ni kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa katika nchi yetu.Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama chetu tumepanga kumpokea na yupo tayari kushirikiana nasi kuwatumikia wananchi,"amesema Dk.Bashiru.

Hata hivyo uamuzi huo wa Lowassa umeonekana kuwakosha wana-CCM kwani baadhi yao wameonesha kufurahia uamuzi huo.

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527