AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUKUTWA NA BANGI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imempandisha kizimbani Mohamed Hamisi (24) kwa shtaka la kukutwa na bangi yenye uzito wa kilo 0.57.


Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Bonifasi Lihamwike, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Veronika Mtafia alidai kuwa Januari 10, mwaka huu eneo la Sinza Kwa Mori, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam mshtakiwa alikutwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya huku akijua ni kinyume cha sheria.


Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo huku upande wa Jamhuri ukisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.


Hakimu Alihamwike alisema hatampa mshtakiwa dhamana kutokana na kurudishwa mara nne mahakamani kwa shtaka hilo moja.


“Kutokana na mtuhumiwa kurudishwa mara nne mahakamani kwa wakati tofauti kwa tuhuma ya kukutwa na dawa za kulevya, mahakama imeamua kutompa dhamana kwa kesi hiyo mpaka hukumu itakapotolewa,” alidai Lihamwike.


Mshtakiwa alirudishwa rumande hadi kesi yake itakaposomwa tena Machi 25, mwaka huu.


Wakati huo huo, mahakama imempadisha kizimbani Emmanuel Mushi (34) Mkazi wa Sinza, Wilaya ya Kinondoni kwa shtaka la wizi.


Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, Wakili wa Serikali, Neema Mushi alidai mnamo Novemba 15, mwaka jana eneo la Kibamba, Wilaya ya Ubungo, aliiba simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh 360,000, pesa taslimu Sh 5,000,000 na pochi moja yenye vitambulisho mali ya Imani Kisiwa.


Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo huku upande wa Jamhuri ukisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.


Hata hivyo, Hakimu Kiliwa alisema kuwa dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaotoa bondi ya Sh milioni 2.7.


Mshtakiwa aliachiwa hadi Aprili 3, mwaka huu kesi yake itakaposomwa baada ya kukidhi masharti ya dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post