SIMBA YAENDELEZA UBABE..YAICHAPA AFRICAN LYON 3-0


Simba SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Kwa ushindi huo, Simba SCinayofundishwa na kocha Mbelgiji Patrick Aussems inafikisha pointi 42 baada ya kucheza mechi 17 ikiendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam FC yenye pointi 50 za mechi 24 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 58 baada ya kucheza mechi 23.

Katika mchezo wa leo mabao ya Simba SC yamefungwa na washambuliaji, Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mawili, moja kila kipindi na linguine Adam Salamba.

Bocco aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya 28 baada ya Emmanuel Semwanza kuunawa mpira uliopigwa na Pascal Wawa kutoka upande wa kulia.

Adam Salamba akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya akimalizia mpira uliotemwa na kipa Douglas Kisembo kufuatia shuti la Nahodha, John Raphael Bocco.

Dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu akimalizia krosi nzuri ya kiungo chipukizi Rashid Juma kutoka upande wa kushoto.

Baada ya bao hilo, African Lyon ikamtoa kipa Douglas Kisembo na nafasi yake kuchukuliwa na Tony Charles aliyekwenda kumalizia vizuri mchezo kwa kutoruhusu mabao zaidi.

Kikosi cha African Lyon kilikuwa; Douglas Kisembo/Tony Charles dk49, Halfan Mbarouk/Adil Nassor dk52, Omary Salum, Roland Msonjo, Emmanuel Semwanza, Jabir Aziz, Pato Ngonyani, Awadh Juma, Stephano Mwasyika, Said Mtikila na Ramadhani Chombo ‘Redondo’/Benedictor Jacob dk55.

Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Pascal Wawa/Yussuf Mlipili dk82, Muzamil Yassin, Hassan Dilunga/Abdul Suleiman dk86, Haruna Niyonzima, Adam Salamba, John Bocco na Rashid Juma/Jonas Mkude dk74.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Coastal Union imelazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Azam FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Coastal Union walitangulia kwa bao la Ayoub Lyanga dakika ya 45 na ushei kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Azam FC dakika ya 51.
Nayo Mwadui FC wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya jirani zao, Biashara United ya Mara Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga.

Mabao yote ya Mwadui FC yamefungwa na mshambuliaji wake tegemeo, Salim Aiyee dakika ya 45 na 64, wakati la Biashara United limefungwa na Waziri Junior kwa penalti dakika ya 50.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post