NYOKA WA AJABU AUA WATU WATANO SUMBAWANGA..HUUA SIKU ZA JUMAPILI

Na Gurian Adolf -Sumbawanga

Maofisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wameamua kushirikiana na mtaalamu wa tiba za jadi wa kijiji cha Kinambo, Tarafa ya Milepa, kumsaka nyoka wa ajabu anayedaiwa kuua watu watano kwa nyakati tofauti kijijini hapo. 

Diwani wa Kata ya Milepa wilayani Sumbawanga, Aporinali Macheta, alisema jana kwamba, nyoka huyo aina ya koboko anadaiwa kugonga na kusababisha vifo vya watu watano katika kipindi cha miaka minne tofauti.

Alisema jambo la kushangaza ni kwamba nyoka huyo amekuwa na kawaida ya kugonga watu kila mwaka katika moja ya siku ya Jumapili. 

Alisema siku kama hiyo ya Jumapili mwaka 2016 nyoka huyo aliwagonga watu wawili ambao walifariki dunia muda mfupi baadaye.

Alisema kuwa msako dhidi ya nyoka huyo umeanza baada ya juzi kumgonga na kumsababishia kifo Ndoti (60), mkazi wa Kijiji cha Kinambo, ambaye alifariki muda mfupi baada ya kugongwa na nyoka huyo.

Alisema nyoka huyo anapatikana katika mti mmoja wa mwembe ambapo baada ya kumgonga mtu hutokomea porini.

Macheta aliongeza kuwa baada ya tukio hilo wanakijiji walimwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuomba wataalamu wa Maliasili ambao walifika kijijini hapo jana. 

Alisema walifika na kuanza kuendesha msako dhidi ya nyoka huyo kwa kumtumia kijana aitwaye Seif Sikanda, ambaye ni mtaalamu wa tiba za asili.

“Msako wa nyoka huyo unaendelea, lakini leo (jana) tulifanikiwa kumuua kwa risasi nyoka mdogo mwenye urefu wa futi saba aina ya koboko... tunaendelea kumsaka yule mkubwa ambaye ndio tishio la maisha ya wananchi wa kijiji hiki,” alisema. 

Ofisa Mtendaji wa kijiji hiko, Richard Sungura, alisema pamoja na nyoka huyo kumgonga na kusababisha kifo cha Ndoti, pia amesababisha vifo vya Elezina Kasele (68), Saise Shigela (21), John Mboganzuri (63) na Benedicto Kasele (14). 

Alisema nyoka huyo pamoja na kuua watu hao kwa nyakati fofauti, pia amekuwa aking’ata mifugo kama ng’ombe, mbuzi na mbwa. 


CHANZO- NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527