RAIS WA TFF AITIBUA CHADEMA KAULI YA "TABIA ZA U - TUNDU LISSU', WAMTAKA AOMBE RADHI

 Kauli ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia kumfananisha mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Michael Wambura kwa kupinga hoja, kumeiibua Chadema na kumtaka rais huyo kuomba radhi hadharani.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimetaja mambo manne kinachoazimia kuyatekeleza iwapo Karia hatoomba radhi.

Jumamosi Februari 2, 2019 jijini Arusha katika mkutano mkuu wa TFF Karia alikemea watu wenye tabia za ‘u Tundu Lissu’ katika soka, kwamba kamwe hawezi kukubali kuona wakiendelea kukosoa uongozi wa TFF.

Baada ya mkutano huo Karia alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli hiyo amesema, “Nimesema kama kuna ‘ma Tundu Lissu’ kwenye mpira, nadhani mnaelewa Lissu anahangaika kwenye vyombo vya habari kuikashifu Serikali, na Wambura anazungumza kwenye vyombo vya habari kuikashifu TFF na uongozi wa TFF.”

“Hivyo nikamlinganisha Wambura na Lissu, ila kama hii kauli imewakera wengine naomba samahani.”

Kufuatia kauli hiyo,jana jioni mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alitoa tamko la chama hicho, akimtaka Karia kuomba radhi.

“Tumepokea kauli yenye ukakasi mkubwa (ya Karia) kuwa atawashughulikia wale wote ambao wataleta ‘ U-Tundu Lissu’ kwenye mpira. Kauli hii imebeba ujumbe mahsusi kuwa watu aina ya Tundu Lissu wanastahili kushughulikiwa kwenye sekta zote,“ amesema Mrema.

Amebainisha kuwa chama hicho kinaamini kuwa watu aina ya Lissu ni wale wote wenye mtazamo na uwezo wa kuhoji, wanaotaka utawala wa sheria ufuatwe na wanaotaka sheria na Katiba ziheshimiwe.

“Sasa kauli ya Karia inatufanya tujiulize maswali inawezekana anawajua waliomshughulikia Lissu na ndio maana anataka kuwatumia kushughulikia 'Tundu Lissu' walioko kwenye mpira,” alisema Mrema.

Katika maelezo ya leo ya Chadema, chama hicho kimesema kufuatia kauli hiyo ya Karia kinatafakari kufanya mambo manne ambayo ni; kuhamasisha wanachama wake kutoshiriki matukio ya TFF, kususia bidhaa zote zenye nembo na au zinazotolewa na TFF zikiwemo jezi za timu za Taifa, kuchukua hatua dhidi ya kampuni zitakazoendelea kushirikiana na TFF na kushawishi wadau wa mpira kutoshirikiana na TFF.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post