WANACHAMA WA THRDC KANDA YA ZIWA WALAANI MAUAJI YA WATOTO NJOMBE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI   KULAANI MAUAJI YA WATOTO WASIOKUWA NA HATIA MKOANI NJOMBE 


 1.0 Utangulizi 

Sisi waanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu  (THRDC) Kanda  ya  Ziwa tumesikitishwa sana na  mauaji  ya  watoto kumi (10) yaliyotokea  Mkoani  Njombe (Nyanda  za juu  Kusini) na  kuacha  simanzi kubwa  kwa Taifa, familia, ndugu jamaa na marafiki.  Hivyo  basi  tunaungana  na wapenda  amani wote nchini  kwenye kuomboleza  msiba   huu  wa kitaifa. 

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi na waandishi mbali mbali ambao wamekuwa wakifwatilia suala la mauaji ya watoto hao, chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Watu (waganga) ambao wamekuwa wakihusishwa na imani za kishirikina wamekuwa ni chanzo cha mauaji yaliyotokea mjini Njombe. Waganga hao wamekuwa wakiua wakiteka watoto na kuwaua huku wakichukua sehemu mbali mbali za miili yao. Aidha, jeshi la polisi linaendelea na upelelezi kuhakikisha wauaji hao wanatiwa nguvuni na kujibu mashtaka yatakayowakabili.

Ndugu  Waandishi wa habari  ifahamike  kuwa haki  ya  kuishi ni haki ya msingi  na ya Kikatiba kwa  kila  binadamu. Nchini Tanzania  haki  hiyo inalindwa  na Katiba  yetu  ya  Jamhuri  ya  Muungano wa Tanzania) kupitia  Ibara  ya 14. HIvyo basi kuvunja haki hii ni kukiuka Katiba pamoja na mikataba mbali mbali ya Kimataifa ambayo Tanzania ni nchi mwanachama.

Ndugu  waandishi,  mauaji  yaliyotokea  Mkoani Njombe  siyo  ya  kufumbiwa  macho   kwani kitendo  hicho  ni uhalifu   mkubwa   unaokiuka msingi  wa  haki ya  kuishi  na  utu wa  binadamu. Katika taifa  letu  hakuna  mwenye  mamlaka  ya  kuiondoa  roho  ya  binadamu  mwingine isipokuwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Hata hivyo, historia yetu kama taifa la Tanzania japo bado tuna sheria inayomruhusu Rais kusaini adhabu ya kifo, ni mara chache sana tumeshuhudia marais wetu wastaafu na rais aliyepo madarakani wakisaini adhabu hii ya kifo. Ni dhahiri kwamba, suala la kutoa uhai wa mtu ni jambo baya kutokea katika taifa letu.

 2.0 Ulinzi wa Mtoto Kisheria 

Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 kifungu cha 9 inasema; mtoto ana haki ya KUISHI kujaliwa utu wake, kuheshimiwa, kupumzika (kucheza), kuwa huru, kuwa na afya bora, kupata elimu pamoja na makazi kutoka kwa wazazi wake.

 Hata hivyo, jukumu hili la ulinzi wa maisha ya mtoto lipo pia Kikatiba na katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kila mtu ana wajibu wa kulinda na kuteteta Katiba na sheria za nchi. 

Ipo pia mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama ambayo imeweka haki mbali mbali za mtoto ikiwemo haki ya kuishi. Baadhi ya Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa kuhusu watoto wa mwaka 1989, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Haki za Kiraia wa mwaka 1966, Nyongeza ya Mkataba wa Maputo wa Mwaka 2003. 

Mikataba yote hii na mingine inaelekeza juu ya haki za watoto na ulinzi wa utu wao.

Ndugu waandishi  mauaji ya  watoto  kumi  ni  ukatili  mkubwa, kwani uhai  wa watoto hawa  umekatisha  ghafla maisha na ndoto zao  na kuleta  simanzi kubwa  kwa  ndugu  jamaa , marafiki  na taifa  kwa  ujumla. Taifa limepoteza kizazi ambacho kingeweza kulitumikia kwa maslahi mapana ya nchi.

Ndugu waandishi wa habari, Ikumbukwe kuwa watoto ni kundi ambalo kwa namna moja ama nyingine hawawezi kupata haki zao bila ya msaada wa watu wengine. Hivyo basi, inapotokea kundi hili la watoto linaathirika na matendo ya kinyama kama haya ya mauaji, ni jukumu letu sote kukemea vikali na kupaza sauti zetu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wauaji wa watoto hawa.

 Hivyo basi, nyinyi kama waandishi wa habari na sisi watetezi wa haki za binadamu naomba tushikamane katika kipindi hiki kuwasemea watoto na kuhakikisha haki na utu wao unalindwa wakati wote.

3.0 Wito Wetu
Jeshi la polisi lifanye uchunguzi wa kina na kuwabaini wote waliohusika na mauaji tajwa na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika na mauaji hayo.

Vyombo  vya  ulinzi  na usalama  viwe macho  na  waganga  wanaohusisha   utajiri/mafanikio  na  vitendo  vya  kishirikina na kuwachukulia hatua stahiki pindi wanapokiuka sheria na Katiba ya nchi.

Waandishi wa habari watumie  kalamu  zao  kwenye  kutoa  elimu kwa  jamii  juu  ya  athari  za ushirikina ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa kero kwa jamii na kusababisha hasara na simanzi kwa ndugu, jamaa, marafiki na taifa kwa ujumla.

Jamii  ishiriki  kikamilifu  kwenye  kuripoti  viashiria  vya ushirikina na uvunjifu wa haki za binadamu katika jamii.
Tamko   hili limetolewa na wanachama wa Mtandao wa  Watetezi wa Haki za Binadamu  kanda  ya  Ziwa.

 Mashirika  Wanachama 
OJADACT
ADLG
WOTE SAWA
SAUTI YA WANAWAKE  UKEREWE
UVUUMA 

Na Edwin Soko

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post