TFDA YAJIVUNIA KUIPAISHA TANZANIA KWA KUWA NA MIFUMO BORA YA UDHIBITI WA BIDHAA

NA WAMJW-Dar es Salaam
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema katika kipindi Cha Miaka mitatu imeweza kufanya mambo mbalimbali ya udhibiti wa usalama, ubora na usalama wa bidhaa za ndani na nje ya Nchi ikiwemo kutambulika kimataifa kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya ISO 9001: 2015.


Hii ni kutokana na mafanikio ya miaka mitatu ya utekelezaji wa kazi chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii nchini.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Adam Fimbo amebainisha hayo wakati akitoa ripoti ya miaka mitatu ya Mamlaka hiyo wakati wa ziara maalum ya Maafisa Mawasiliano na habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.


“Kutokana na kuwa na mifumo thabiti ya udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, mnamo Mwezi Desemba 2018, TFDA imetambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vipodozi, ambapo hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hatua hii


Fimbo ameeleza kuwa, TFDA katika mikakati yake hiyo imeweka mifumo na taratibu za ndani za utoaji huduma na utendaji bora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ISO 9001:2015 kwa huduma za kawaida na ISO 17025:2005 kwa huduma za maabara.


Aidha, ameongeza kuwa huduma za TFDA hutolewa kwa kuzingatia viwango vya Mkataba wa Huduma Wateja kama ulivyorejewa mwaka 2016.


“Mfumo wa usajili wa bidhaa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo idadi ya bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi vilizosajiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, katika kipindi cha 2015/16 hadi 2017/18.


Pia tumesajili jumla ya bidhaa 14,345 kutoka bidhaa 8,866 zilizokuwa zimesajiliwa mwaka 2015/16 ambapo ni sawa na ongezeko la 62%. Hii imetokana na kuongezeka kwa uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara na kukua kwa biashara.” Ameeleza Fimbo.


Aidha, Fimbo ameongeza kuwa TFDA imekuwa ikifanya tathmini na usajili wa bidhaa kwa lengo la kuhakiki endapo bidhaa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi kabla ya kuruhusiwa katika soko.


“Kuwepo kwa bidhaa nyingi zilizosajiliwa katika soko ni uthibitisho kuwa walaji wanapata bidhaa zilizo salama, zenye ubora na ufanisi.


Pia tumeweza kusajili maeneo ya biashara za bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi kwa lengo la kutambua maeneo ambayo bidhaa hizo zinazalishwa, kuhifadhiwa, kusambazwa na kuuzwa. Mfumo huu husaidia kuhakikisha kuwa maeneo husika yanakidhi vigezo ili kutoathiri usalama, ubora na ufanisi wa bidhaa”. Alieleza Fimbo.


Aidha ameongeza kuwa, TFDA katika kipindi cha miaka mitatu (2015/16 – 2017/18), imeweza kusajili jumla ya maeneo 25,630 ya biashara za bidhaa zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na maeneo 9,000 yaliyosajiliwa mwaka 2016/17 na maeneo 5,606 mwaka 2015/16, hii ikiwa ni sawa na ongezeko la 60.5%.


Aidha, katika kipindi hiki, TFDA imeendelea kushuhudia kufikiwa kwa dira yake ya kuwa taasisi ya mfano barani Afrika katika udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi na hivyo kuvutia nchi mbalimbali kuja kujifunza mifumo iliyopo na kwenda kuitekeleza nchini kwao.


(mfano nchi za Zimbabwe, Rwanda, Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Botswana, Mauritius, Lesotho na Bangladesh zinekuja kujifunza TFDA).


“Katika kipindi cha mwaka 2015/16 – 2017/18, Mamlaka imefanikiwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika utekelezaji wa mipango kazi yake.

Mamlaka katika kipindi cha 2017/18 itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji kwa ufanisi wa malengo mahususi nane (8) yaliyomo katika Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (5) yaani 2017/18 – 2021/22, ili kulinda afya ya jamii.” Alieleza Fimbo.


Mafanikio mengine ni pamoja na kukamilika kwa jengo la Maabara na kufungwa kwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi jijini Mwanza jambo ambalo limesaidia kusogeza huduma zaidi kwa jamii .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527