SEKRETARIETI YA AJIRA YATAKIWA KUTENDA HAKI ILI KUIWEZESHA SERIKALI KUPATA WATUMISHI WENYE SIFA STAHIKI

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetakiwa kuendelea kutenda haki katika kuratibu mchakato wa ajira ili kuiwezesha Serikali kupata watumishi wenye sifa stahiki na maadili mema ambao watatoa huduma kwa umma kwa kuzingatia weledi na kuwajali wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Taasisi za umma.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo iliyopo Magogoni jijini Dar es Salaam, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya Sekretarieti hiyo na kujiridhisha namna Sekretarieti hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo ambacho kinatakiwa kutenda haki ili Serikali ya Awamu ya Tano ipate watumishi wenye sifa na vigezo watakaoendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuliletea taifa maendeleo katika sekta za miundombinu, afya, viwanda, biashara, kilimo, usafiri wa anga, elimu na  uchumi kwa ujumla wake.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, awali Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilikuwa ikilalamikiwa sana kuwa, mchakato wa kuomba kazi Serikalini ulikuwa ukichukua muda mrefu kiasi cha waombaji kusahau kama waliwasilisha maombi, hivyo ameipongeza Sekretarieti kwa kubuni mfumo wa upokeaji wa maombi ya kazi (Recruitment Portal) na mfumo wa kupanga wasailiwa waliofaulu ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na waombaji wa ajira Serikalini na kuongeza kuwa, hivi sasa mchakato wa ajira mpya unachukua siku 52 tu licha ya kuwepo taratibu nyingi zinazozingatiwa kukamilisha mchakato mzima.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, mfumo huo una kanzi data ya waombaji wote waliofanyiwa usaili na kupata ufaulu mzuri lakini kutokana na uwepo wa fursa chache za ajira hawakupangiwa vituo vya kazi, hivyo unaiwezesha serikali kupata watumishi kwa wakati pindi wanapohitajika haraka katika Taasisi za Umma. 

Sanjari na hayo, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameitaka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kutobweteka kwa mafanikio waliyoyapata kupitia mfumo wa Ajira Portal na badala yake waongeze kasi ya ubunifu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kwa dhati kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma nchini.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier M. Daudi, amesema ofisi yake ilianzishwa kwa lengo mahususi la kukabiliana na changamoto za ajira zilizokuwa zikijitokeza hapo awali, hivyo iliundwa ili kuongeza uwazi, kutenda haki na kuhakikisha kuwa ajira zinapatikana kwa kuzingatia sifa.

Bw. Daudi amesisitiza kuwa, ofisi yake kwa kushirikiana na waajiri inazingatia Sera ya Ajira, Sheria, Kanuni na Taratibu katika kusimamia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kuiwezesha Serikali kupata watumishi wenye sifa na maadili mema watakaoisaidia Serikali kufikia malengo yake makubwa iliyojiwekea, ikizingatiwa kuwa watumishi ndio injini ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Mbarak Abdulwakil amemshukuru Mhe. Dkt. Mwanjelwa kwa nasaha zake za kuitaka Sekretarieti kuzingatia weledi katika jukumu zito la kuwezesha ajira za watumishi wa umma na kumhakikishia kuwa, maelekezo yote  aliyoyatoa yatatekelezwa kikamilifu na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inatekeleza majukumu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuifadhi taarifa za wataalam, kutangaza nafasi wazi za kazi zinazojitokeza katika Utumishi wa Umma, kuhusisha wataalam ili kushirikiana nao kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji, kuwashauri waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa ajira, kuandaa orodha ya wahitimu wa vyuo na wataalam kwa weledi kwa madhumuni ya kurahisisha rejea za ujazaji nafasi na kuendesha mchakato wa ajira wa Watendaji Wakuu wa Wakala na Idara zinazojitegemea za Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527