MWANAKIJIJI AMWAGA MABATI NA MADAWATI KWA AJILI YA OFISI YA KIJIJI NA SHULE SHINYANGA

Mkazi wa kijiji cha Ng'hama Juma Masende ametoa msaada wa madawati 61 kwa ajili ya shule ya msingi Ng’hama,mabati 41 kwa ajili ya ofisi ya mwenyekiti wa kijiji cha Ng’hama iliyopo kata ya Mwalukwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. 

Msaada huo umetolewa leo Jumatatu 28,2019 na familia ya Juma Masende ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani  lengo ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa maendeleo na kuondoa changamoto mbalimbali hasa katika idara ya elimu na utawala. 

Akipokea msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 9 Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu aliwataka wananchi kuwa na uchu wa maendeleo kwa kutoa misaada yenye tija kwa jamii ambapo ameitaja idara ya elimu kukabiliwa na changamoto lukuki ambazo zingetatuliwa na wananchi. 

“Wadau wa maendeleo wamekuwa wakisahau kuwekeza kwenye idara ya elimu na badala yake wamekuwa wakijikita na mambo ya anasa huku idara hiyo ikiendelea kudidimia,tubadili mitazamo hiyo tuisaidie serikali na wadau wengine kuiinua idara ya elimu”, alisema Maduhu. 

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Juma Masende, Mwenyekiti wa kijiji cha Ng’hama Philemon Masende alisema msaada huo  uliotolewa na kaka yake, utapunguza changamoto ya upungufu wa madawati kijijini hapo unaosababisha utoro kwa baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wakikaa chini. 

Diwani wa kata ya Mwalukwa Ngasa Mboje aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za kimaendeleo zinazofanyika kwa kushiriki kutoa michango pamoja na nguvukazi pindi zinapohitajika.

TAZAMA PICHA ZA TUKIO HAPA CHINI
 Mwenyekiti wa kijiji cha Ng'hama Philemon Masende ambaye ni kaka yake na mfadhili aliyetoa msaada huo bwana Juma Masende akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wakati wa makabidhiano wa madawati 61 kwa ajili ya shule ya msingi Ng’hama,mabati 41 kwa ajili ya ofisi ya mwenyekiti wa kijiji cha Ng’hama iliyopo kata ya Mwamadilana halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Picha zote na  Malaki Philipo - Malunde1 blog
Philemon Masende (kulia) akikabidhi msaada wa madawati 61 kwa Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu (kushoto) kwa ajili ya kusaidia idara ya elimu na idara ya utawala.
 Madawati 61 ambayo yametolewa na Juma Masende kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto ya madawati katika shule ya msingi Ng'hama.
 Sehemu ya mbele ya jengo la ofisi ya mwenyekiti wa kijiji cha Ng'hama ambalo limeezekwa kwa hisani ya Juma Masende ambaye ametoa mabati 41. 
  Upande wa nyuma ujenzi ukiendelea ofisi ya mwenyekiti wa kijiji cha Ng'hama.
 Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu akiwasisitiza wananchi kuwa na utamaduni wa kuwekeza katika shughuli za kimaendeleo zilizo na tija,hasa kuwekeza katika idara ya elimu.
Wanakijiji wa Ng'hama wakiwa kwenye mkutano wa makabidhiano ya madawati na mabati,wakisikiliza kinachoendelea.
Wanafunzi wa shule ya msingi Ng'hama wakiwa na familia ya Juma Masende.
Familia ya Juma Masende, (kulia) Justina Masende (mtoto), (katikati) Theresa Ruben (mke),  (kushoto) Philemon Masende(kaka) mwenyekiti wa kijiji cha Ng'hama.

Picha zote na  Malaki Philipo - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post