Picha : MKUU WA MKOA NA KATIBU WA CCM SHINYANGA WATUNISHIANA MISULI..BASHIRU AKWEPA KIAINA... AMPA ZIGO LA MGOGORO MAKAMU WA RAIS

Katibu mkuu wa CCM,Dkt. Bashiru Ally akizungumza leo Shinyanga - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
 **
Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dkt. Bashiru Ally amesema atamuomba Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake  CCM (UWT),Bi. Gaudensia Kabaka kusuluhisha mgogoro kati ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Bi. Haula Kachwamba.

Dkt. Bashiru amefikia maamuzi hayo leo Jumatatu Januari 7,2019 wakati akiongea na watendaji wa CCM ngazi ya kata,wilaya na mkoa kwenye Ukumbi wa CCM Shinyanga na kueleza kuwa kitendo cha kutunishiana misuli ya kimamlaka baina ya viongozi hao wa chama na serikali Mkoani ni tishio katika kasi ya ujenzi wa mkoa wa Shinyanga. 

Alisema mgogoro huo hauna nafasi katika kipindi hiki ambapo CCM ina mpango mkakati wa kujiimarisha ili kuondoa changamoto za maendeleo zinazowakabili wananchi. 

"Hapa nimeambiwa kuna ka mgogoro kati ya Mkuu wa mkoa na katibu wa CCM mkoa,nimesikitika sana, siyo kawaida,ingawaje watu wanasema wanawake hawapendani,lakini mimi nina ushahidi wanawake ni msingi wa umoja kokote,wanawake huvumilia sana,wanawake ndiyo mfano bora katika jamii...

"Sasa nimeambiwa jambo hilo mwenyekiti (Mabala Mlolwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga) limeshamshinda…mwanaume!!…..nasikia hata Waziri Mkuu (Kasimu Majaliwa) amekuja hapa limemshinda....mwanaume!!, nasikia hata Makamu wa pili wa rais ambaye ni Mlezi wa mkoa huu,Mjumbe wa kamati kuu ya siasa (Balozi Seif Idd) amesema limemshinda…mwanaume! Sasa mimi sitaki kuliingilia kwa sababu na mimi ni mwanaume ",alisema Dkt. Bashiru.

“Jambo hili namkabidhi Mjumbe wa Kamati kuu na makamu wa Rais mwanamke,na nitamuongezea nguvu,nitamwambia Mama Kabaka,Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake,wakae wajifungie,wanawake wanne,wawili waliotofautiana na wawili nitakaowaomba wawasuluhishe... 

…..mimi nitapokea taarifa na taarifa hiyo nitampelekea Mwanaume Mkuu wetu,Rais Wetu kwa sababu yeye ndiye aliyemteua mkuu wa mkoa,na yeye ndiye aliyeniteua mimi ninayemuajiri katibu wa mkoa,hivyo tutakaa sisi wanaume wawili kumaliza matatizo ya wanawake hawa wawili”,aliongeza Dkt. Bashiru. 

“Na ninaamini wanawake wawili nitakaowaomba na wanaume wawili tutakaolishughulikia kulimaliza,ngoma itakuwa sare sare,sisi hatuishiwi ubunifu kwa kuimarisha umoja na mshikamano katika chama chetu...

…bila mkuu wa mkoa wewe siyo lolote siyo chochote,bila katibu wa mkoa wewe siyo lolote siyo chochote,wewe unasimamia shughuli za serikali ya CCM,wewe unasimamia chama ambacho ndicho kinasimamia serikali ya CCM,mkianza kuyumba mtayumbisha mkoa mzima,nimeshayasikia ya kila upande na sijazungumza nao tangu nimefika,kila mara nilikuwa nakwepa nisimsikie huyu wala huyu.... 

“Kwa sababu ninazo taarifa za kutosha,taarifa hizo ntamkabidhi Makamu wetu wa Rais na Mjumbe wa kamati kuu Mama Kabaka,wakae wawasikilize halafu watatushauri na matarajio yangu ni kwamba jambo hilo litakwisha salama,sasa kwa sababu ni mchakato ninawaomba kuanzia leo,wafanye zoezi dogo tu,washikane mikono mbele yangu na nyie mkishuhudia,muwe mashahidi halafu habari ya ushauri wa hawa akina mama wawili itafuata baadae”,alisema Dkt. Bashiru. 

Katika hatua nyingine,Dkt. Bashiru alisema pia katika mkoa wa Mwanza kuna mgogoro akidai upo mvutano kati ya kundi la Anthony Diallo (Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro) na Meck Sadick (Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza) na kusisitiza kuwa hahitaji kuona vurugu bali umoja na mshikamano. 

Dkt. Bashiru aliwakemea viongozi wenye dhamana ya kuunganisha wanachama na wananchi kuhusishwa na upuuzi wa namna yoyote,akidai kuwa hata hisia tu kwa sababu wamebeba dhamana ya kujenga chama,taifa, umma hivyo hawapaswi kuhusishwa kwa namna yoyote ile na mgogoro wa aina yoyote ile unaomhusu mtu yeyote. 

“Ikianza kuzoeleka tabia hiyo,mamlaka ya Urais na mwenyekiti wetu yatadhoofishwa,ofisi ya katibu mkuu wa chama itadharauliwa na huo utakuwa mwanzo wa kufaranganyika kwa uongozi wa chama na serikali,hizi ni dhamana nzito na sisi dhamana zetu,ni dhamana tulizozibeba kutokana na wananchi”,alisema. 

Na Kadama Malunde – Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Bi. Haula Kachwamba wakikumbatiana baada ya kutakiwa  Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally kushikana mikono ili kumaliza mgogoro wao.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Bi. Haula Kachwamba wakiendelea kukumbatiana kumaliza tofauti zao.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack (kushoto)  na Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Bi. Haula Kachwamba wakiangaliana baada ya kumaliza kukumbatiana walipotakiwa kushikana mikono.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Bi. Haula Kachwamba wakionesha hali ya furaha baada kutakiwa kushikana mikono kumaliza tofauti zao.

Wakuu wa wilaya na viongozi mbalimbali wa CCM wakiwa ukumbini.

Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na viongozi mbalimbali wa CCM wakiwa ukumbini.
Mkutano ukiendelea.
Wabunge wakiteta jambo. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini,Stephen Masele akifuatiwa na Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga,Mbunge wa jimbo la Msalala,Ezekiel Maige na Mbunge wa jimbo la Kahama Mjini,Jumanne Kishimba wa kwanza (kulia).

Mkutano unaendelea.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack akizungumza ukumbini.
 wa CCM mkoa wa Shinyanga, Bi. Haula Kachwamba akizungumza ukumbini.

Mkutano unaendelea.

Wanachama wa CCM wakiwa ukumbini.
Wanachama wa CCM wakiwa wamesimama wakati wa kufunga mkutano.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527