ASKOFU KAKOBE AWATAKA VIONGOZI WA CHADEMA WALIOTUKANA VIONGOZI WA DINI WATUBU


Askofu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship nchini Tanzania, Zachary Kakobe, amewataka viongozi wa CHADEMA waliotoa maneno machafu kwa viongozi wa dini kutubu haraka iwezekanavyo, la sivyo chama chao kitatumbukia shimoni.

Mchungaji Kakobe ametoa kauli hiyo leo kwenye ibada aliyokuwa akiendesha kanisani kwake Mwenge, Jijini Dar es salaam, ambapo amesema kwamba viongozi hao wanatakiwa wajue kuwa viongozi wa dini wana nguvu kuliko wanavyodhani, hivyo ni vyema wakaomba msamaha kwa walichokifanya, kwani kuwatukana viongozi wa dini ni utovu wa nidhamu ni kiburi.

"Baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Rais Magufuli na viongozi wa dini, kuna baadhi ya viongozi wa siasa wa CHADEMA tena walioko katika baraza kuu waliwatukana viongozi wa dini kupitia mitandao ya kijamii, wajue viongozi wa dini wana nguvu katika nchi hii kuliko wao wanavyodhani. 

Viongozi ambao wamewatukana viongozi wa dini kwenye mitandao ya kijamii wanapaswa kutubu haraka sana, wakikaidi agizo hilo chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu ambalo hakitainuka tena, kuwatukana viongozi wa dini kwa sababu hawakuzungumza yale mliyotaka kuyasikia ni utovu wa nidhamu ni kiburi", amesema Askofu Kakobe.

Ikumbukwe kwamba wiki iliyopita Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alikutana na viongozi wa dini zote Ikulu jijini Dar es salaam na kuufanya nao mazungumzo juu ya kero zinazowakabili katika maeneo yao, huku akiwaomba kuelimisha jamii na kuwa na hofu ya Mungu.

Via>>EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post