RC MWANRI AIAGIZA BODI YA PAMBA KUNUNUA PAMBA YA WAKULIMA

Na Tiganya Vincet
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagiza Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kuhakikisha inanunua pamba iliyobaki Daraja B (fifi) ya wakulima wa Urambo ili kutowakatisha tamaa ya kuendelea na kilimo hicho.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kufuatia malalamiko kutoka kwa wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Itengamatwi wilayani Urambo juu ya uwepo wa pamba ambao hadi hivi sasa iko katika maghala na wakulima hawajalipwa fedha.


Aliwataka wakulima kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa jitihada zinaendelea ili kuhakikisha pamba yao fifi(daraja B) ambayo hadi hivi sasa bado iko katika maghali ya kuhifadhi mazao inanunuliwa na Bodi ya Pamba Tanzana baada ya wanunuzi wa awali kusimamisha ununuzi na kuzima mashine.


Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wakulima kuzingatia kanuni 10 za kilimo cha zao hilo ili kuepuka kuzalisha pamba Daraja B ambalo ndio wakati mwingine linakuwa kigezo cha wanunuzi kuwapa bei mbaya na wakati mwingine kukataa kununua pamba yao.


Alisema azimo la Mkoa wa Tabora katika msimu wa kilimo cha zao ujao ni kila mkulima ni lazima azingatite kanuni kumi za zao hilo ikiwemo kuvuna kwa wakati na kuhifadhi katika hali ya usafi.


Mwanri alisema hatua hiyo itasaidia kulinda ubora wa zao hilo na kumsaidia mkulima kupata Daraja A na kulipwa bei ya juu itakayompa fedha nyingi ambazo zitasaidia kuboresha maisha yake.


Kwa upande wa Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Modest Kaijage aliwahakikishia wakulima wa pamba wilayani Urambo ambao wana pamba fifi(Daraja B) kuwa Bodi imeamua kuinunua na itawalipa malipo yao.


Alisema Mkurugenzi Mkuu wa TCB amesema kuwa wanafanya utaratibu ili waweze kununua pamba iliyobaki ambapo wao ndio wataifanyia uchambuzi kwa ajili ya msimu ujao.


Awali baadhi ya wakulima walisema kuwa walipokuwa wakihamasishwa kulima pamba na wakati wa ununuzi waliambiwa kuwa pamba ina madaraja mawili lakini wakati wa mauzo pamba yao daraja B haikununuliwa na bado ipo katika maghali jambo linalowakatisha tamaa kuendelea na kilimo hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post